Home Habari za michezo RUDIGER ATUHUMIWA KUMPIGA ALVARO CARRERAS MAZOEZINI

RUDIGER ATUHUMIWA KUMPIGA ALVARO CARRERAS MAZOEZINI

0

MADRID, HISPANIA: HALI ya sintofahamu ndani ya Real Madrid imezidi kuwa mbaya baada ya kufichuliwa kwa jina la mchezaji aliyedaiwa kupigwa na beki Antonio Rudiger katika ugomvi uliotokea mazoezini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania, beki huyo Mjerumani alijawa na hasira kiasi cha kumpiga mchezaji mwenzake ambaye sasa ametambulika kuwa ni Alvaro Carreras, kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Betis wiki mbili zilizopita. Inadaiwa kuwa wachezaji walilazimika kuingilia kati kuwatenganisha wawili hao.

Carreras, 23, alitoa tamko akijaribu kutuliza hali, akieleza tukio hilo halikuwa kubwa na tayari limetatuliwa.

Ripoti pia zinaeleza kuwa baada ya tukio hilo, Rudiger aliomba radhi na hata kuwakaribisha wachezaji pamoja na familia zao kwenye chakula maalum kama ishara ya kuomba msamaha.

Hata hivyo, tukio hilo ni sehemu ya mlolongo wa migogoro inayokikumba kikosi cha Real Madrid msimu huu huku chumba cha kubadilishia nguo kikitajwa kugawanyika.

Nyota wa timu hiyo, Kylian Mbappe, naye amekuwa katikati ya lawama hizo, akidaiwa kuingia kwenye mabishano na mmoja wa wasaidizi wa kocha Alvaro Arbeloa wakati wa mazoezi.

Inasemekana Mbappe alizungumza kwa hasira na kutumia maneno yasiyofaa kwa msaidizi huyo aliyekuwa akisimamia mazoezi.

Mbappe pia alikosolewa baada ya kusafiri kwenda mapumzikoni Sardinia akiwa na mpenzi wake, Ester Exposito, wakati wachezaji wenzake wakiendelea na maandalizi ya mechi muhimu dhidi ya Barcelona.

Hatua hiyo imezua hasira kwa mashabiki, ambapo zaidi ya watu 250,000 wamesaini ombi la mtandaoni wakitaka nyota huyo aondoke klabuni hapo. Wengi wanaamini kuwa tangu ajiunge na Real Madrid mwaka 2024, timu hiyo haijapata mafanikio makubwa yaliyotarajiwa.

Hata hivyo, upande wa Mbappe umetetea safari yake, ukieleza kuwa ratiba hiyo ilisimamiwa na madaktari wa klabu kutokana na kuuguza majeraha hivyo hajakiuka utaratibu wowote.