BIRMINGHAM, ENGLAND: KATIKA usiku mdogo wa Ulaya, macho yote ya mashabiki wengi wa soka yataelekezwa Villa Park ambapo Aston Villa watakuwa na kibarua kizito cha kupindua matokeo dhidi ya Nottingham Forest kwenye mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Europa League.
Timu hizo mbili zote zinacheza Ligi Kuu England.
Forest watashuka dimbani wakiwa na faida ndogo ya bao 1-0 kutoka mchezo wa kwanza lakini historia na mazingira ya mchezo huo wa marudiano vinatoa taswira kwamba hakuna mwenye uhakika wa kutinga fainali hivyo mechi ipo wazi bado kwa pande zote mbili.
Aston Villa wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa katika kipindi kigumu kuelekea mwisho wa msimu, kipigo cha mabao 2-1 walichopata dhidi ya Tottenham mwishoni mwa wiki kilikuwa ni cha tatu mfululizo katika mashindano yote, hali inayotia shaka juu ya ubora wao katika wakati huu muhimu.
Matokeo hayo pia yanaendeleza mfululizo mbaya ulioanza na kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Forest, jambo linalofuta kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mechi tisa mfululizo waliokuwa nao awali katika michuano hii ya Europa League. Hata hivyo, rekodi yao nyumbani katika Europa League msimu huu ni ya kutisha, wakishinda michezo yote sita waliyocheza Villa Park, jambo linalowapa matumaini ya kurejea kwenye ubora wao.
Kwa upande wa Nottingham Forest, wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na morali ya hali ya juu. Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Chelsea uliopatikana mwanzoni mwa wiki uliwaongezea nguvu, ukiwa ni ushindi wao wa tano mfululizo katika mashindano yote. Matokeo hayo yamewapa utulivu kwenye ligi ya England na kuwapa nafasi ya kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo huu. Forest wameonyesha uimara mkubwa katika hatua za mtoano, wakipambana hadi dakika za ziada dhidi ya Midtjylland kabla ya kuiondoa Porto kwa jumla ya mabao 2-1.
Uwezo wao wa kucheza vizuri ugenini umeonekana wazi, kwani hawajapoteza mechi yoyote ya ugenini katika hatua za mtoano msimu huu.
Kihistoria, Aston Villa wanaonekana kuwa na makali wanapokutana na Forest katika uwanja wao, wakishinda mechi nne zilizopita za nyumbani dhidi yao. Hata hivyo, kwa ujumla katika mechi za hivi karibuni, ushindani umekuwa mkali zaidi huku Forest wakionyesha uwezo wa kuhimili presha, hasa wanapokutana na timu za England katika michuano ya Ulaya ambapo bado hawajapoteza. Katika takwimu za kuvutia, Villa wamekuwa wakifunga mabao mawili au zaidi katika kila moja ya mechi zao tano za mwisho za nyumbani kwenye Europa League, ishara kwamba wana uwezo mkubwa wa kushambulia wanapokuwa mbele ya mashabiki wao.
Kwa upande mwingine, Forest wamekuwa hatari zaidi kwenye mipira ya adhabu, wakiwa ndiyo timu iliyofunga penalti nyingi zaidi katika michuano hii msimu huu, jambo linaloweza kuwa silaha muhimu katika mchezo wa aina hii wenye presha kubwa.
Wachezaji muhimu wanaotarajiwa kuamua hatma ya mchezo huu ni pamoja na Emiliano Buendía kwa upande wa Villa mwenye mabao mawili na asisti nne katika michuano hii pamoja na Ollie Watkins mwenye mabao manne na asisti moja huku kwa Forest macho yakielekezwa kwa Igor Jesus mwenye mabao saba na asisti moja.
Hata hivyo, timu zote mbili zinaingia kwenye mchezo huu zikiwa na changamoto za majeruhi ambazo zinaweza kuathiri mipango ya makocha wao. Villa watakosa huduma ya Boubacar Kamara na Amadou Onana huku Forest ikiwakosa Ola Aina, Murillo na Ibrahim Sangare.
Nusu fainali nyingine ya Europa League itapigwa pale Freiburg ambapo wenyeji watakapowakaribisha Braga wakihitaji kupindua matokeo ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza.
Hii ni nafasi muhimu kwa Freiburg kuandika historia kwa kufika fainali ya mashindano haya huku Braga wakisaka kurejea hatua hiyo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2010/11.
Freiburg wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa katika hali isiyoridhisha kiushindani. Sare waliyoipata dhidi ya Wolfsburg mwishoni mwa wiki imewafanya waendelee kukosa ushindi katika mechi nne mfululizo, jambo linaloonyesha kuporomoka kwa kiwango katika kipindi hiki.
Hata hivyo, nguvu yao kubwa imekuwa nyumbani ambapo wamekuwa na rekodi bora sana katika Europa League, wakikaribia kufikia rekodi ya ushindi wa mechi mfululizo 11 za nyumbani.
Ufanisi wao wa kufunga mabao umeonekana wazi, wakifunga wastani wa karibu mabao matatu kwa kila mechi katika michezo yao ya hivi karibuni ya nyumbani kwenye mashindano haya.
Kwa upande wa Braga, wanawasili wakiwa na faida ya mabao lakini pia wakiwa na tahadhari kutokana na historia ya timu za Ureno kushindwa kulinda ushindi wa kwanza katika hatua za juu za mashindano haya.
Hata hivyo, kiwango chao cha hivi karibuni kinatoa matumaini, wakiwa wamepoteza mechi moja kati ya tisa zilizopita katika mashindano yote.
EUROPA CONFERENCE
Katika nusu fainali ya Conference League, Crystal Palace wanarejea nyumbani wakiwa na mtaji mzuri wa mabao mawili baada ya ushindi wa jumla wa mabao 3-1 dhidi ya Shakhtar Donetsk, hali inayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu fainali.
Hii ni nafasi adhimu kwa Palace kuandika historia mpya katika michuano ya Ulaya, hasa wakizingatia kuwa hii ni safari yao ya kwanza kubwa katika michoano hiyo. Katika mchezo mwingine, Strasbourg wanarejea nyumbani wakiwa na presha kubwa baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Rayo Vallecano.
Timu hiyo ya Ufaransa imeingia kwenye kipindi kigumu baada ya kupoteza mechi nne kati ya tano zilizopita katika mashindano yote, hali iliyozima ndoto zao za kushinda mataji mawili msimu huu.
Kuporomoka kwa kiwango hicho kumeathiri pia nafasi yao katika ligi ya ndani, jambo linalowalazimu kuweka nguvu zote katika mashindano ya Conference League.