VITA ya kuwania taji la mchezaji mwenye pasi nyingi za mabao kwenye Ligi Kuu ya NBC 2025/26 imezidi kupamba moto kadri msimu unavyoelekea ukingoni.
Nyota wa timu mbalimbali wanaendelea kuonyesha ubora wao wa kutengeneza nafasi, huku ushindani ukiwa mkubwa kati ya Simba, Yanga na Azam FC.
Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Elie Mpanzu, ameendelea kuwa gumzo baada ya kupanda hadi nafasi ya pili kwenye orodha ya wachezaji wenye pasi nyingi za mabao (Most Assists).
Mpanzu sasa ana assist saba, hatua iliyomfanya kumpiku nyota wa Yanga, Allan Okello, aliyeshuka hadi nafasi ya tatu akiwa na assist sita.
Mabadiliko hayo yameongeza presha kwenye mbio hizo, hasa kwa kuwa kileleni bado anaongoza kiungo mahiri wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, mwenye assist nane. Tofauti ya assist moja tu kati yake na Mpanzu inaifanya vita hiyo kuwa wazi kabisa kuelekea mwisho wa msimu.
Katika nafasi ya nne yupo kiungo wa Yanga, Duke Abuya, ambaye pia ana assist sita sawa na Okello, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa uliopo kwenye eneo la ubunifu na utengenezaji wa mabao kati ya timu hizo tatu kubwa nchini.
Kupanda kwa Mpanzu ni habari njema kwa Simba pamoja na mashabiki wake, hasa ikizingatiwa kuwa nyota huyo alianza msimu kwa kiwango kisichoridhisha ukilinganisha na alivyomaliza msimu uliopita.
Hata hivyo, katika mechi za hivi karibuni ameonekana kurejea kwenye ubora wake, akionyesha uwezo mkubwa wa kuona nafasi na kutoa pasi za mwisho zenye madhara kwa wapinzani.
Ubora wake wa sasa umeongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba, huku akiwa mmoja wa wachezaji wanaotegemewa zaidi katika kutengeneza nafasi za mabao.
Kadri ligi inavyozidi kwenda ukingoni, ushindani wa assist unaonekana kuwa mkali zaidi, na kila mechi inaweza kubadilisha msimamo wa vita hiyo ya ubunifu uwanjani.