Home Habari za michezo YANGA YATIBUA USINGIZI WA SIMBA SC, YAMUWINDA WINGA WA IVORY COAST

YANGA YATIBUA USINGIZI WA SIMBA SC, YAMUWINDA WINGA WA IVORY COAST

0

WAKATI dirisha kubwa la usajili bado halijafunguliwa rasmi, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC wameanza kuonyesha dalili za kufanya maboresho makubwa kikosini kuelekea msimu ujao.

Taarifa zinaeleza kuwa Yanga imeanza kufuatilia kwa karibu huduma ya winga hatari kutoka Ivory Coast, Amani Kouadiokan Michel Breygeneve, anayekipiga katika klabu ya AFAD-Plateau.

Nyota huyo ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji wanaovutia zaidi katika Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu wa 2025/26.

Akiichezea AFAD-Plateau kama winga wa kulia, Amani ameonyesha kiwango bora kwa kufunga mabao 10 na kutoa pasi sita za mabao ndani ya mechi 24 za ligi.

Takwimu hizo zimeifanya Yanga kuvutiwa na uwezo wake, huku ikitajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazofuatilia kwa karibu maendeleo ya mchezaji huyo ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia.

Amani anasifika kwa kasi yake, uwezo wa kupenya mabeki pamoja na kutumia miguu yote miwili kwa ufanisi, jambo linalomfanya kuwa tishio kubwa kwa safu za ulinzi za wapinzani.

Mara nyingi hupenda kuanzia mashambulizi upande wa kulia kabla ya kukata kuingia ndani, akitengeneza nafasi za kufunga au kumalizia mwenyewe kwa ustadi mkubwa. Ni aina ya mchezaji anayebeba hatari muda wote akiwa uwanjani kutokana na ubunifu wake na uwezo wa kubadili matokeo ndani ya dakika chache.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tayari baadhi ya wadau wa soka wameanza kuitahadharisha Ligi Kuu Tanzania Bara juu ya uwezo wa nyota huyo iwapo dili lake la kutua Yanga litakamilika.

Hatua ya Yanga kuanza mapema harakati za usajili inaonekana kuwa sehemu ya mpango wa kuijenga upya timu hiyo kuelekea msimu mpya, hasa baada ya klabu hiyo kuachana na aliyekuwa kocha mkuu, Pedro Gonçalves.

Uongozi wa Yanga unaonekana kutaka kuongeza ushindani kikosini kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kubeba matokeo katika mechi muhimu, huku Amani akitajwa kuwa mmoja wa majina yanayopewa uzito mkubwa katika mipango hiyo.