Home Habari za michezo BARKER AANZA USAJILI KWA KASI, BANCE APEWA KIPAUMBELE SIMBA

BARKER AANZA USAJILI KWA KASI, BANCE APEWA KIPAUMBELE SIMBA

0

UONGOZI wa Simba SC umeanza harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, huku Kocha Mkuu, Steve Barker, akitajwa kuanza kupendekeza baadhi ya majina ya wachezaji anaotaka kusajiliwa katika dirisha kubwa la usajili.

Miongoni mwa majina yaliyo kwenye rada za Wekundu wa Msimbazi ni kiungo mshambuliaji wa klabu ya Marumo Gallants, Ibrahim Bancé, ambaye amekuwa akifuatiliwa kwa karibu kutokana na kiwango chake kizuri akiwa kwenye ligi ya Afrika Kusini.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya michezo zinaeleza kuwa Simba imeanza mawasiliano ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili nyota huyo, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya kikosi kinachotarajiwa kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.

Inaelezwa kuwa pendekezo la usajili huo limetokana na Barker mwenyewe, ambaye ameridhishwa na uwezo wa Bancé katika eneo la kiungo, hasa upande wa ubunifu, kasi na uwezo wa kusaidia mashambulizi.

“Bancé ameonyesha kiwango kizuri akiwa Marumo Gallants. Ana uwezo wa kucheza kwa ubunifu na kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji, jambo ambalo limeifanya Simba kuvutiwa naye,” kilisema chanzo cha karibu na klabu hiyo.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mazungumzo kati ya Simba na menejimenti ya mchezaji huyo tayari yameanza, huku ikielezwa kuwa Bancé anatarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, hali inayoweza kurahisisha dili hilo kukamilika.

Simba inaendelea kufanya tathmini ya kikosi chake baada ya msimu huu kuwa na ushindani mkubwa, huku uongozi wa klabu ukiweka wazi dhamira ya kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuongeza ushindani na ubora ndani ya timu hiyo.

Iwapo usajili huo utakamilika, Bancé ataungana na orodha ya nyota wa kimataifa waliowahi kutua Msimbazi kwa lengo la kuisaidia Simba kutimiza malengo yake ya kutwaa mataji makubwa ndani na nje ya Tanzania.