MCHEZO wa kesho kati ya Coastal Union na Yanga SC umeanza kuchemka mapema kwa vita vya maneno, baada ya Coastal Union kutamba kuwa ipo tayari kuwapa wakati mgumu mabingwa hao watetezi katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema kikosi chake kitaingia uwanjani kikiwa na morali kubwa na bila hofu yoyote mbele ya Yanga, huku akisisitiza kuwa maandalizi yao yamekamilika kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
Coastal Union wanakabiliwa na kibarua kizito cha kuizuia Yanga kupata pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa, lakini Fikiri anaamini timu yake ipo tayari kuonyesha ushindani mkubwa dhidi ya Wananchi.
Amesema ndani ya siku mbili zilizopita, kikosi chake kimetumia muda huo kufanya maboresho muhimu na kuandaa mbinu maalum zitakazowasaidia kukabiliana na ubora na uzoefu wa Yanga.
“Sisi kama Coastal Union tumejiandaa vizuri kabisa. Tumepata nafasi ya kufanya maboresho kadhaa na kuandaa mbinu zetu kuelekea mchezo huu huku tukitambua ubora na uzoefu wa Yanga,” amesema Fikiri.
Kocha huyo amesema wanafahamu presha waliyonayo Yanga katika mbio za ubingwa, lakini pia Coastal Union ina malengo yake ya kuhakikisha inamaliza msimu katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
“Tunafahamu Yanga watakuja kwa lengo la kutafuta ushindi, lakini nasi tupo tayari kupambana. Watakuja kuuliza maswali na Coastal Union tutakuwa tayari kuyajibu. Tunategemea mchezo mzuri wenye ushindani mkubwa,” amesema.
Fikiri ameongeza kuwa morali ya wachezaji wake ipo juu kuelekea pambano hilo, akieleza kuwa ana imani kikosi chake kina uwezo wa kupata matokeo chanya dhidi ya vigogo hao wa Dar es Salaam.