Home Habari za michezo YANGA YAPANGA KUREJESHA MBINU ZA NABI

YANGA YAPANGA KUREJESHA MBINU ZA NABI

0

BAADA ya kuachana na Kocha Mkuu Pedro Gonçalves, mabosi wa Yanga SC wameingia kwenye mbio za kimyakimya kusaka mrithi wa haraka atakayeshika usukani wa timu hiyo, huku jina la kocha Mtunisia, Khalil Ben Youssef likitajwa kuwa chaguo la kwanza kurejea Jangwani.

Siku chache tu baada ya tetemeko la kumfuta kazi Pedro Mei 6, 2026, Yanga imeanza rasmi mchakato wa kutafuta kocha mpya wa kuiongoza timu hiyo kuelekea malengo ya msimu ujao.

Uongozi wa Wananchi haukutaka kupoteza muda, na taarifa zinaeleza kuwa jina la kwanza lililowekwa mezani ni la Muarabu huyo raia wa Tunisia, Khalil Ben Youssef.

Pedro Gonçalves aliondolewa Jangwani saa chache baada ya kuiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC, ushindi uliokuwa wa mwisho kwake ndani ya klabu hiyo.

Katika kipindi chake cha uongozi, Pedro aliiongoza Yanga kwenye jumla ya mechi 35 za mashindano yote tangu alipochukua mikoba ya Romain Folz Oktoba 28, 2025. Hata hivyo, licha ya ushindi huo dhidi ya KMC, inaonekana viongozi wa klabu hiyo walikuwa tayari wamefikia uamuzi wa kuachana naye.

Khalil Ben Youssef si jina jipya kwa mashabiki wa Yanga. Kocha huyo aliwahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Nasreddine Nabi, kipindi ambacho Yanga ilifanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/23 hadi kufika fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Ingawa hakudumu kwa muda mrefu Jangwani, Ben Youssef aliacha kumbukumbu nzuri kutokana na utulivu wake, maarifa ya mbinu na mchango wake mkubwa katika mafanikio ya timu hiyo barani Afrika.

Sasa Yanga inaamini kurejea kwake kunaweza kuwa suluhisho la haraka, hasa kutokana na uzoefu wake na uelewa mkubwa wa mazingira ya klabu hiyo.