KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga SC, Abdihamid Moallin amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC, huku akibainisha kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu.
Moallin amesema maandalizi ya timu hiyo yamekamilika kwa kiwango kizuri, huku wachezaji wakiwa kwenye hali bora kiakili na kimwili kuelekea mchezo huo ambao ameutaja kuwa na umuhimu mkubwa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema morali ya kikosi ipo juu na kila mchezaji anatambua wajibu wake ndani ya uwanja, jambo ambalo linawapa imani ya kufanya vizuri na kupata matokeo chanya mbele ya Coastal Union.
“Wachezaji wako kwenye morali nzuri na tunajua huu ni mchezo muhimu sana kwetu. Tunaamini tutakwenda uwanjani kutoa kiwango bora na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Moallin.
Kocha huyo amesema kwa sasa benchi la ufundi limeamua kuelekeza nguvu zote kwenye mchezo mmoja mmoja badala ya kuangalia malengo ya muda mrefu, huku akisisitiza kuwa ushindi dhidi ya Coastal Union ndiyo kipaumbele chao kikubwa kwa sasa.
Moallin amesema Yanga kama mabingwa watetezi wa ligi kwa misimu minne mfululizo wana jukumu la kuendelea kuonyesha soka la kiwango cha juu litakalowavutia mashabiki pamoja na kuendeleza ushindani wao kwenye ligi.
“Mashabiki wetu wanapenda soka la kushambulia na la kuvutia. Kikosi chetu kimejengwa kwa ajili ya kucheza mpira wa kushambulia, kushinikiza juu na kucheza kwa kasi,” amesema.
Moallin ameongeza kuwa malengo yao ni kuutawala mchezo kwa dakika zote 90, huku akiahidi kuwa timu hiyo itapambana kwa nguvu zote kuhakikisha inaondoka na ushindi mbele ya Coastal Union.