Home Habari za michezo VILLA YAPINDUA MEZA KWA FOREST, KUIKABILI FREIBURG FAINALIEUROPA

VILLA YAPINDUA MEZA KWA FOREST, KUIKABILI FREIBURG FAINALIEUROPA

0

ASTON Villa imezamisha matumaini ya Nottingham Forest ya kutinga fainali ya Europa League baada ya kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 4-0 uliowasogeza karibu zaidi kumaliza ukame wa miaka 30 bila taji kubwa.

Mabao mawili ya kuchelewa ya John McGinn yaliongeza lile la penalti la Emi Buendia pamoja na bao la ufunguzi la Ollie Watkins, yameifanya Villa kupindua meza dhidi ya Forest baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita.

Villa sasa itakutana na Freiburg kwenye fainali itakayochezwa Istanbul nchini Uturuki, Mei 20, 2026 baada ya klabu hiyo ya Bundesliga kuiondoa Braga kwa jumla ya mabao 4-3.

Kocha wa Villa, Unai Emery, anawania taji lake la tano la Europa League, baada ya kujiunga na klabu hiyo akiwa tayari na rekodi kubwa katika michuano hiyo.

Villa sasa inalenga kutwaa taji kubwa la kwanza tangu waliposhinda Kombe la Ligi mwaka 1996, ambalo pia linaweza kuwapa nafasi ya kucheza UEFA Champions League msimu ujao.

Villa bado inashika nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu England, na iwapo itamaliza hapo pamoja na kushinda Europa League, timu ya sita ambayo kwa sasa ni AFC Bournemouth nayo itafuzu Champions League.

Ulikuwa ushindi wa kustahili kwa Villa mbele ya mashabiki wao, akiwemo Prince William, huku Forest wakionekana kutokuwa na tishio kubwa bila Morgan Gibbs-White.

Kiungo huyo mshambuliaji alikuwa benchi baada ya kuumia kichwani kwenye ushindi wa Jumatatu dhidi ya Chelsea, jeraha lililohitaji kushonwa nyuzi nyingi.

Villa ilifanikiwa kusawazisha jumla ya mabao dakika saba kabla ya mapumziko, pale Watkins alipomalizia krosi ya Buendia kutoka upande wa kushoto.

Dakika 13 baada ya kipindi cha pili kuanza, Villa iliongeza bao la pili baada ya mwamuzi Glenn Nyberg kutoa penalti kufuatia mapitio ya VAR, ambapo Nikola Milenkovic alionekana kumvuta Pau Torres.

Watkins pia alifunga bao ambalo baadaye lilikataliwa kwa kuotea, huku kipa Emiliano Martínez akiokoa hatari ya Chris Wood upande wa Forest, kabla ya McGinn kufunga mabao mawili ya haraka yaliyohitimisha ushindi huo mkubwa.

FREIBURG 3-1 BRAGA 
Ushindi wa jumla wa mabao 4-3, umeifanya SC Freiburg kufuzu fainali yao ya kwanza kabisa ya michuano ya Ulaya baada ya kuifunga SC Braga waliobaki na wachezaji 10 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Europa League uliochezwa Alhamisi, Mei 7, 2026.

Ikiwa mbele kwa jumla ya mabao 2-1 kutoka mchezo wa kwanza, Braga ilipata pigo kubwa baada ya Mario Dorgeles aliyefunga bao la ushindi la dakika za mwisho nchini Ureno kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea faulo ya makusudi Jan-Niklas Beste.

Freiburg haikuchukua muda kutumia faida hiyo ya idadi ya wachezaji, wakitangulia kuongoza kupitia tukio lililoanzia kwa Jean-Baptiste Gorby kushindwa kuokoa mpira vizuri, uliogonga goti la Lukas Kubler kabla ya kuingia wavuni ukigusa mwamba wa mbali.

Ingawa bao la kwanza lilikuwa na bahati kidogo, hapakuwa na bahati yoyote kwenye bao la pili la kuvutia la Yohan Manzambi dakika nne kabla ya mapumziko.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20, alijitengenezea nafasi nje ya eneo la penalti na kupiga shuti kali la mguu wa kulia lililojaa wavuni kona ya mbali, jambo lililosababisha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Freiburg ndani ya Uwanja wa Europa-Park Stadion.

Victor Gomez aliugonga mwamba baada ya kumpita kipa wa Freiburg Noah Atubolu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, huku Vincenzo Grifo naye akizuiwa na mwamba huo kwa shuti la chini mapema kipindi cha pili.

Kipa wa Braga Lukas Hornicek aliokoa hatari mbili za kushangaza dhidi ya Igor Matanovic na Matthias Ginter dakika 20 kabla ya mwisho, lakini hakuwa na la kufanya wakati Kubler alipoongeza bao la tatu kwa kichwa kikali.

Bao la kichwa la karibu la Pau Victor liliwapa Braga matumaini dakika saba baadaye, lakini timu hiyo ya kocha Carlos Vicens haikuweza kurejea mchezoni.

Kocha Julian Schuster ushindi wake huo ulikuwa wa 11 mfululizo kwa Freiburg nyumbani katika Europa League, ikisawazisha rekodi ya muda wote iliyowekwa na Sevilla FC kati ya Aprili 2014 na Machi 2016.