Home Habari za michezo VITA YA UINGEREZA NA WAHISPANIA CONFERENCE LEAGUE KUAMULIWA UJERUMANI, REKODI ZIKIWEKWA

VITA YA UINGEREZA NA WAHISPANIA CONFERENCE LEAGUE KUAMULIWA UJERUMANI, REKODI ZIKIWEKWA

0

CRYSTAL Palace ya England, imeandika historia mpya ya klabu baada ya kuifunga Shakhtar Donetsk na kutinga fainali ya kwanza kabisa ya michuano ya Ulaya katika UEFA Conference League.

Palace iliingia kwenye mchezo wa marudiano ikiwa mbele kwa mabao 3-1 baada ya ushindi ilioupata wiki iliyopita nchini Poland, na ilidhani imeongeza bao lingine kupitia kwa Yeremy Pino aliyefunga kwa utulivu baada ya kupokea pasi ya Jean-Philippe Mateta. Hata hivyo, bao hilo lilikataliwa kutokana na kuotea kwa tofauti ndogo sana.

Katika mazingira ya shamrashamra kubwa ndani ya dimba la Selhurst Park, Palace ilipata bao la kuongoza dakika ya 25. Shuti kali la Adam Wharton lilipanguliwa na kipa Dmytro Riznyk, lakini mpira ulimkuta Daniel Munoz ambaye alitoa pasi ya chini iliyoishia kujaa wavuni baada ya Pedro Henrique kujifunga.

Shakhtar ilijibu na kusawazisha bao hilo kupitia Equinaldo aliyepokea pasi ya Pedro Henrique kabla ya kupiga shuti maridadi lililojaa moja kwa moja kona ya juu ya lango.

Kabla ya mapumziko, Mateta alikaribia kuirejeshea Palace uongozi wa mabao matatu kwa jumla, lakini mpira uligonga mwamba

Katika kipindi cha pili, Ismaila Sarr aliihakikishia Palace ushindi wa jumla wa mabao 5-2 baada ya kufunga bao la pili kufuatia krosi ya chini kutoka kwa Tyrick Mitchell. Bao hilo lilikuwa la tisa kwake kwenye mashindano hayo msimu huu, na sasa ndiye kinara wa mabao wa Conference League.

Sasa Crystal Palace itavaana na Rayo Vallecano ya Hispania kwenye fainali itakayochezwa Mei 27, 2026 mjini Leipzig, baada ya timu hiyo ya Hispania kuiondoa Strasbourg kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0 kwenye nusu fainali nyingine.