SIMBA BADO INATAKA UBINGWA, YAICHAPA MTIBWA 3-0
SIMBA SC imeendelea kuonyesha dhamira ya kupambana hadi mwisho katika mbio za kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro..
Wekundu wa Msimbazi walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza mapema dakika ya tisa kupitia kwa Rushein De Reuck aliyefunga kwa mkwaju wa penalti uliowapa Simba mwanzo mzuri wa kutawala mchezo.
Baada ya bao hilo, Simba waliendelea kulisakama lango la Mtibwa Sugar wakitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, huku wenyeji wakijitahidi kusawazisha matokeo bila mafanikio.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba wakiwa mbele kwa bao 1-0, matokeo yaliyowapa utulivu na kuingia vyumbani wakiwa na faida muhimu.
Waliporejea kipindi cha pili, Simba waliongeza kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 77 kupitia kwa Seleman Mwalimu aliyemalizia vizuri pasi safi kutoka kwa Anicet Oura.
Bao hilo lilizidi kuwavunja nguvu Mtibwa Sugar ambao walishindwa kuhimili presha ya Simba katika dakika za mwisho za mchezo.
Dakika ya 90, Anicet Oura alihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu na kuweka muhuri wa ushindi wa mabao 3-0, matokeo yanayoifanya Simba kuendelea kuifukuzia Yanga katika mbio za ubingwa huku ligi ikielekea ukingoni.