BELLINGHAM, SIKUSTAHILI KUWA NYOTA WA MCHEZO
BAADA ya timu ya taifa ya England kulazimishwa sare ya bila kufungana na Ghana, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jude Bellingham amesema hakustahili kuwa nyota wa mchezo huo badala yake tuzo hiyo ilipaswa kwenda kwa mmoja wa wachezaji wa timu pinzani.
Katika mechi hiyo Bellingham alikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo ambao alikiri kupitia wakati mgumu wa kuivunja safu ya ulinzi ya Ghana jambo ambalo anaamini hakustahili tuzo kutokana na ubora wa wapinzani wao.
“Kusema ukweli sikustahili (tuzo hii). Pengine ilipaswa kwenda kwa mmoja wa vijana wao ambao walizuia vizuri sana,” amesema Bellingham huku akikiri kuwa ilikuwa vigumu kwake kuingia na kutawala mchezo kama alivyozoea.
Nyota huyo wa Real Madrid ameipongeza Ghana kwa kutimiza mpango mkakati wa kutafuta na hatimaye kupata sare ambayo inaweza kuwasaidia kusonga mbele.
Amekiri kuwa timu hiyo ilifanya kazi nzuri ya kuzuia mashambulizi ya England na ilistahili matokeo hayo kutokana na nidhamu ya kuzuia.
Kiungo huyo pia amegusia namna timu hiyo inavyopata wakati mgumu wa kutafuta matokeo kwenye mechi ya pili ya mashindano jambo aliloliita kuwa ni homa ya mechi.
Ameeleza kuwa ni kawaida kwa England kushinda mchezo wa kwanza na kufanya vizuri, lakini inapofika mechi ya pili mambo huwa magumu na kuishia kupata sare.
“Ni homa ya mechi ya pili, si ndivyo? tukiwa na England, tunashinda ya kwanza, tunafanya vizuri na kisha tunatoka sare mechi ya pili,” ameongeza kiungo huyo
Kauli ya Bellingham inaonyesha namna ambavyo England imekuwa na historia ya kupata wakati mgumu katika mechi za pili za mashindano makubwa.
Rekodi za tangu 2016 zinaonyesha kwenye mechi nane za mashindano tofauti England kwenye mechi ya pili imeshinda mechi mbili tu dhidi ya Wales kwenye Euro 2016 ikishinda mabao 2-1 na Panama kwenye Kombe la Dunia 2018 ikishinda 6-1, mechi nyingine zikiisha kwa sare.
Katika mashindano ya Euro 2020, England ilitoka sare tasa dhidi ya Scotland baada ya kuanza kwa ushindi dhidi ya Croatia, hali iliyojirudia Kombe la Dunia 2022 walipolazimishwa sare ya 0-0 na Marekani.
Mwaka 2024 kwenye Euro timu hiyo ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Denmark na kwenye Kombe la Dunia 2026 imeendeleza rekodi hiyo baada ya sare ya bila kufungana.