Yanga SC

AZAM WALOESHWA ZANZIBAR, BACCA AVUA AIBU NYUMBANI

Vardo June 24, 2026 6:14 pm

YANGA imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo uliopigwa Visiwani Zanzibar.

Mabingwa hao watetezi walionekana kuwa na nia ya kulipa kisasi mapema kufuatia matokeo ya awali yaliyowagharimu katika michuano mingine, huku wakitawala sehemu kubwa ya mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga.

Bao la kwanza la Yanga lilifungwa dakika ya 41 na Ibrahim Bacca aliyemalizia pasi nzuri kutoka kwa Prince Dube, bao lililowapa utulivu vijana hao kuelekea mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 1-0.

Kipindi cha pili Yanga iliendelea kushambulia kwa kasi zaidi na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 73 kupitia kwa Laurindo Depu aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya mwamuzi kuamua kuwepo kwa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Pacome Zouzou aliihakikishia Yanga ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 81, akihitimisha kazi nzuri ya kikosi hicho kilichoonyesha ubora mkubwa mbele ya Azam FC.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujihakikishia nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiendeleza matumaini ya kutetea taji hilo ambalo ndilo pekee lililosalia mikononi mwao msimu huu.

Matokeo hayo yanaonekana kuwa kisasi cha michezo iliyopita ambapo Yanga ilipoteza mataji ya Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho baada ya kukwama mbele ya Azam FC.

Safari hii, Wanajangwani wameonyesha tofauti kwa kuibuka na ushindi uliowarejeshea heshima na kuongeza morali katika mbio za ubingwa.

MUUNDO RAHISI NA UBUNIFU WA KISASA NDANI YA MERIDIANBET ICY FRUITS SIMBA BADO INATAKA UBINGWA, YAICHAPA MTIBWA 3-0