MSEMAJI wa Yanga SC, Ally Kamwe amesema kuondoka kwa kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama, kuliiacha timu yao na pengo kubwa eneo la kiungo mshambuliaji kutokana na ubora wake mkubwa wa kucheza nafasi ya namba 10 kwa kiwango cha juu.
Chama aliondoka Yanga baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika kabla ya kurejea Simba SC. Nyota huyo aliwahi kujiunga na Wananchi akitokea Simba na kufanikiwa kuonyesha kiwango kizuri akiwa ndani ya kikosi hicho.
Kamwe amesema Yanga ilikuwa na bahati ya kuwa na viungo wawili wabunifu wenye uwezo mkubwa, Stephane Aziz Ki na Chama, jambo lililoifanya timu hiyo kuwa na ushindani mkubwa eneo la ubunifu na ushambuliaji.
Ameeleza kuwa baada ya Aziz Ki kuuzwa kwenda Wydad Casablanca na Chama kuondoka mwishoni mwa mkataba wake, Yanga ililazimika kuingia sokoni kutafuta mbadala wa uhakika wa nafasi hiyo muhimu.
“Eneo ambalo naweza kukiri limetusumbua ni namba 10. Ilitusumbua baada ya kumchukua Mohammed Doumbia, kwa sababu alitakiwa kuingia moja kwa moja kwenye timu kutokana na kukosekana kwa mbadala wa nafasi hiyo,” amesema.
Kamwe amesema Chama ameendelea kuthibitisha ubora wake mkubwa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wengi wakimtazama kama mchezaji wa kiwango cha juu kutokana na uwezo wake wa kubadili matokeo ya mchezo na kuiongoza timu katika nyakati muhimu.
Ameongeza kuwa Yanga ilikuwa ikifuatilia kwa karibu mwenendo wa Chama na kuvutiwa na kiwango chake, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni maamuzi binafsi ya mchezaji huyo kuhusu mustakabali wake wa kisoka baada ya mkataba wake kumalizika.
Kamwe amesisitiza kuwa kupewa kwa Chama mkataba wa mwaka mmoja haikuwa ishara ya kupunguziwa thamani au heshima, bali ilikuwa sehemu ya mipango ya klabu iliyozingatia muda wake wa kucheza pamoja na malengo ya muda mrefu ya Yanga SC.