MSEMAJI wa Yanga SC, Ally Kamwe amesema ushindani dhidi ya Simba SC msimu huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na msimu uliopita, hali iliyofanya dabi ya Kariakoo kuwa ngumu zaidi na yenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka nchini.
Kamwe amesema tofauti ya matokeo kati ya misimu hiyo miwili inaonyesha wazi namna ushindani ulivyobadilika, akibainisha kuwa msimu huu Yanga imekusanya pointi mbili pekee katika michezo dhidi ya Simba, tofauti na msimu uliopita ambapo ilitwaa alama zote sita.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Simba ya sasa imeimarika zaidi katika maeneo mbalimbali ya kikosi jambo linaloongeza ushindani mkubwa kila timu zinapokutana uwanjani.
Amesema maboresho hayo yanaonekana wazi kuanzia safu ya ushambuliaji hadi ushindani wa ndani ya mchezo wenyewe.
“Kiwango cha ushindani kilichopo sasa ni tofauti kabisa na kilivyokuwa msimu uliopita, hata eneo la winga limekuwa na maboresho makubwa,” amesema Kamwe.
Amefafanua kuwa msimu uliopita Simba walikuwa na Joshua Mutale katika nafasi ya winga, lakini kwa sasa uwepo wa Anicet Oura umeongeza ubora mkubwa zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
“Ukimuangalia Mutale na sasa Oura kuna tofauti kubwa sana. Simba wameimarika na ushindani wao umeongezeka hata ndani ya uwanja,” amesema Kamwe alipokuwa akizungumzia maendeleo ya wapinzani wao hao wa jadi.
Pamoja na kuongezeka kwa ushindani huo, Kamwe amesema Yanga itaendelea kupambana kuhakikisha inarejea kwenye kiwango chake bora dhidi ya Simba, huku akisisitiza kuwa malengo yao ni kuendelea kupigania mafanikio na kuwapa furaha mashabiki wa klabu hiyo.