MABAO mawili ya dakika ya 18 na 63 ya kiungo nyota wa Yanga, Allan Okello, sambamba na lile la dakika ya 75 kutoka kwa Maxi Nzengeli, yametosha kuipa timu hiyo pointi tatu dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Bao la kwanza Okello alilifunga baada ya kupokea pasi ya Prince Dube na kufanya kwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili pasi ya Pacome Zouzoua ikamkuta Okello akiwa nje kidogo ya boksi, akaachia shuti lililomshinda kipa wa Coastal Union, Chuma Ramadhan na kujaa wavuni.
Baadaye Okello akamuwekea pasi nzuri Maxi aliyehitimisha ushindi huo na kumfanya Okello sasa kufikisha mabao matano na asisti saba.
Ushindi huo kwa Yanga wa mabao 3-0, ni wa kwanza kwa Kaimu Kocha Mkuu, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’, tangu alipoteuliwa kukiongoza hicho hicho Mei 6, 2026, akichukua nafasi ya Mreno, Pedro Goncalves.
Uongozi wa Yanga ulitangaza kuachana na Pedro, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ishinde bao 1-0 dhidi ya KMC FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, akidumu ndani ya kikosi hicho kwa siku 193, tangu alipotambulishwa rasmi, Oktoba 25, 2025.
Tangu alipotambulishwa, Pedro aliiongoza Yanga katika jumla ya mechi 19 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo alishinda 14 na kutoka sare tano, huku timu hiyo ikifunga mabao 44 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
Hadi anaondoka Pedro Yanga msimu wa 2025-2026, ilikuwa imecheza mechi 21, za Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo ilishinda 15 na kutoka sare sita, ikifunga mabao 47 na kuruhusu matano, ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 51.
Baada ya kuondoka kwa Pedro, Yanga ikamtangaza Kocha, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’, kukaimu nafasi hiyo huku akirejea tena ndani ya kikosi hicho kufuatia kuondoka awali Julai 27, 2025, alipohudumu Mkurugenzi wa Ufundi. Moalin anashirikiana na Patrick Mabedi aliyekuwa msaidizi tangu mwanzo wa msimu alipokuwa Kocha Romain Folz kisha Pedro.
Kocha huyo Mmarekani mwenye asili ya Somalia, alirejea Yanga Machi 23, 2026, akihudumu kocha msaidizi wa Pedro, akiwa na uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania, baada ya awali kuzifundisha pia timu mbalimbali zikiwemo za Azam FC na KMC FC.
Ushindi wa leo kwa Yanga unaifanya kuendeleza kijikita kileleni mwa msimamo na pointi 54, baada ya kucheza mechi 22 za Ligi Kuu hadi sasa.
Kwa upande wa Coastal Union, hii ni mechi ya pili mfululizo kupoteza, baada ya Mei 5, 2026, kuchapwa mabao 3-2, ugenini dhidi ya Fountain Gate.
Pia kichapo hicho kwa Coastal Union ni cha pili kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias, tangu alipoteuliwa Aprili 10, 2026, akichukua nafasi ya Mohamed Muya aliyeondoka Aprili 8, 2026.
Fikiri alianza kwa ushindi mechi mbili za mwanzo kwa kuzichapa Dodoma Jiji mabao 3-1, kisha Singida Black Stars 2-1, akianza vyema majukumu yake ndani ya kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’.
Baada ya hapo akachapwa mechi mbili mfululizo akianza na kichapo cha mabao 3-2, dhidi ya Fountain Gate, kisha kuchapwa 2-0 na Yanga, zote ikicheza kwenye viwanja vya ugenini.
Kocha huyo alikuwa hana timu ya kufundisha Ligi Kuu tangu alipoachana na KenGold FC, Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya mwenendo mbaya wa Ligi Kuu, jambo lililosababisha kushuka daraja hadi Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026.
Coastal Union msimu huu imecheza mechi 22 hadi sasa, ikishinda tano, sare saba na kupoteza 10, ikishika nafasi ya 12 na pointi 22.
Coastal Union imeendeleza unyonge dhidi ya Yanga kwani hata mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa Desemba 7, 2025, ilishindwa kutamba na kuchapwa bao 1-0.
Katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja Jamhuri, jijini, Dodoma, bao la Yanga lilifungwa na mshambuliaji, Prince Dube dakika ya 88.