KICHAPO cha mabao 4-1, ilichokipata Azam FC, dhidi ya TRA United katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Mei 8, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kimekifanya kikosi hicho kuvunjiwa rekodi nne.
Katika mechi hiyo, mabao ya TRA United yalifungwa na Ammy Mapaka mawili, huku Ally Ng’anzi na Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ wakifunga bao moja kila mmoja wakati la kufutia machozi Azam lilifungwa na Jephte Kitambala.
Rekodi ya kwanza iliyovunjwa Azam ni kucheza mechi 25 za Ligi Kuu Bara bila kupoteza tangu ilipochapwa na Yanga 2-1, Aprili 10, 2025, ikiwa imedumu siku 393 (sawa na mwaka mmoja na siku 28).
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, mabao ya Yanga yalifungwa na nyota wa kikosi hicho, Pacome Zouzoua dakika ya 11 na Prince Dube dakika ya 34, huku lile la Azam likifungwa na Lusajo Mwaikenda dakika ya 81.
Kabla ya kichapo hicho, Azam ilicheza mechi 25 za Ligi Kuu tangu Aprili 10, 2025, ambayo ni msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hizo ilishinda 15 na kutoka sare 10, rekodi iliyovunjwa na TRA United ya kucheza muda mrefu bila kupoteza.
Rekodi ya pili iliyovunjwa kwa Azam, ni ya kupoteza mechi ya kwanza msimu huu wa 2025-2026, ya Ligi Kuu, kwani kabla ya hapo timu hiyo ilicheza 21, ikishinda 11 na kutoka sare 10 na kuiachia Yanga ambayo ndio pekee tu haijapoteza hadi sasa.
Kama haitoshi, rekodi ya tatu kwa Azam FC iliyovunjwa ni ya kupoteza mechi ya kwanza ya ugenini msimu huu wa 2025-2026, kwani kabla ya kichapo hicho ilicheza jumla ya mechi 11 za Ligi, ambapo kati ya hizo ilishinda tano na kutoka sare sita.
Rekodi ya nne iliyovunjwa ni kuruhusu idadi kubwa ya mabao kwani kabla ya hapo mechi iliyoruhusu mabao mengi ni ya sare ya 2-2, ugenini dhidi ya Pamba Jiji, Machi 2, 2026, ikionyesha wazi safu ya kujilinda ilikuwa ni nzuri.
Akizungumzia kipigo hicho, Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge alisema licha ya kuanza mechi vizuri walikosa mwendelezo na kuruhusu wapinzani wao kutengeneza mashambulizi mengi.