Habari za michezo
BAO LA DABI LAMFUNGULIA CHAMA MILANGO YA URAIA TANZANIA
Vardo
May 10, 2026
9:26 am
BAO la kipekee alilofunga kiungo mshambuliaji wa Simba SC, raia wa Zambia, Clatous Chama, katika dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga limeanza kuzaa matunda nje ya uwanja baada ya Serikali kuanza kuangalia uwezekano wa kumpatia uraia wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya soka nchini.
Hatua hiyo imewekwa wazi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyesema Serikali imeanza kupitia taratibu za awali za kutathmini namna ambavyo Chama anaweza kupata uraia wa Tanzania kufuatia kiwango chake bora na ushawishi mkubwa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Makonda ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za wanamichezo bora iliyoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa, ambapo alimpongeza nyota huyo wa Simba kwa mchango wake mkubwa katika kukuza ushindani wa soka la Tanzania kupitia kiwango chake cha hali ya juu akiwa Simba SC na hapo awali Young Africans SC.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, bao la ufundi alilofunga Chama dhidi ya Yanga katika dabi ya Kariakoo limekuwa sehemu ya mjadala mkubwa wa kisoka ndani na nje ya nchi, huku wengi wakivutiwa na uwezo wake mkubwa wa kubadili matokeo katika mechi muhimu.
“Kutokana na ubora wake, wizara imeanza kuangalia taratibu za kumpatia uraia ili kuongeza ushindani na ubora wa timu yetu ya taifa. Chama ameonyesha kiwango cha kipekee na ni mchezaji anayebadili matokeo muda wowote,” amesema Makonda.
Chama ameendelea kujijengea heshima kubwa Tanzania kutokana na uwezo wake wa kucheza mechi kubwa na kuamua matokeo kwa ubunifu wake wa kipekee.
Bao lake alilofunga kwenye mchezo wa Kariakoo Derby ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam, limeendelea kuwa gumzo duniani na kutajwa miongoni mwa mabao bora yaliyofungwa msimu huu.