Habari za michezo
KIUNGO WA YANGA AWEKA WAZI DHAMIRA YA KUTWAA TAJI
Vardo
May 10, 2026
9:31 am
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga SC, Allan Okello amesema yupo tayari kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha timu yake inaendelea kupata matokeo chanya katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Okello alitoa kauli hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa jana dhidi ya Coastal Union uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, ambapo aliifungia Yanga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0.
Nyota huyo raia wa Uganda amesema ushindi huo ni matokeo ya ushirikiano mkubwa uliopo ndani ya kikosi hicho, huku akisisitiza kuwa kila mchezaji amekuwa akipambana kuhakikisha timu inapata pointi muhimu katika kila mchezo.
Okello amesema furaha yake kubwa ni kuona Yanga ikiendelea kusonga mbele kwa ushindi mfululizo, jambo ambalo linaongeza morali kwa wachezaji na benchi la ufundi kuelekea hatua za mwisho za msimu.
“Malengo ya timu hiyo bado ni kutetea ubingwa wao, hivyo hatupaswi kulegea licha ya kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, kwani ushindani wa msimu huu ni mkubwa na kila mchezo una umuhimu wake,” amesema.
Kiungo huyo pia aliwaomba mashabiki wa Yanga kuendelea kuiunga mkono timu yao katika kipindi hiki muhimu cha msimu, akiamini sapoti yao imekuwa chachu kubwa ya mafanikio ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata uwanjani