Habari za michezo
OURA AREJEA KAZINI, ATUMA SALAMU KWA WAPINZANI
Vardo
May 10, 2026
9:36 am
WINGA wa Simba, Anicet Oura amerejea rasmi uwanjani baada ya kupona jeraha lililomuweka nje katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Oura alipata majeraha hayo wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Yanga ambapo alishindwa kumaliza dakika 90 za mchezo huo kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Seleman Mwalimu aliyefanikiwa kuisaidia Simba kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Kutokana na majeraha hayo, nyota huyo alikosa michezo miwili muhimu ya Simba, ikiwemo dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga iliyochezwa Mei 3, 2026 pamoja na mchezo dhidi ya JKT Tanzania.
Akizungumza baada ya kurejea mazoezini, Oura amesema tayari yupo katika hali nzuri na ameanza kazi ya kuisaidia timu yake kupambana katika michezo iliyobaki msimu huu.
“Niko fiti na nimerejea kazini kwa ajili ya kupambania nembo ya Simba kwa kufikia malengo yanayotarajiwa,” amesema Oura.
Simba sasa inaendelea na maandalizi ya michezo yake tisa iliyosalia katika Ligi Kuu Bara, huku kurejea kwa Oura kukiongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho kinachowania ubingwa msimu huu..