WINGA wa KMC, Erick Mwijage amesema wameumizwa na uamuzi wa mwamuzi kushindwa kuipa timu hiyo penalti ya wazi kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga walipopoteza kwa bao 1-0 akieleza kilichotokea ni ukatili kwa timu inayopambana kujinusuru.
Kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 6, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, wakati Mwijage akipambana kuelekea kufunga, beki wa Yanga, Chadrack Boka alionekana kumuangusha ndani ya boksi, lakini haikutasfiriwa kama penalti.
Licha ya hivyo, Mwijage alisema kupoteza mchezo huo wameshasahau na sasa wanaangalia mechi tisa za mbele wakihitaji kufanya vizuri ili kujinusuru na janga la kushuka daraja.
Kufungwa na Yanga, ni matokeo ambayo yamezidi kuiweka KMC mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku ikiambulia pointi tisa ikicheza mechi 21, ikishinda mbili, sare tatu na imepoteza 16.
Akizungumza na Soka la Bongo, Mwijage alisema katika kipindi ambacho KMC inapitia wakati mgumu wa kusaka matokeo mazuri, maamuzi kama hayo yanaongeza ugumu zaidi kwa timu yao ambayo bado inapigania kubaki salama kwenye ligi.
Alisema wachezaji wa KMC waliamini walistahili kupata penalti katika mchezo huo lakini mwamuzi aliamua kuendelea na mchezo jambo lililowaumiza ndani ya uwanja.
“Kwa kweli ilikuwa penalti ya wazi kabisa, lakini maamuzi yakawa tofauti. Inaumiza hasa kwa timu ambayo inapambana kujitafuta kama sisi,” alisema Mwijage.
Pamoja na malalamiko hayo, nyota huyo alisema bado hawajakata tamaa huku akisisitiza kitu muhimu kwa sasa ndani ya kikosi hicho ni wachezaji kuendelea kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki kigumu.
Alisema presha ya matokeo ipo lakini wamekubaliana kupambana pamoja hadi mwisho wa msimu kuhakikisha wanaitoa KMC kwenye mazingira hayo magumu.
“Kikubwa kwa sasa ni kuendelea kuishi pamoja kama timu. Hiki ni kipindi kigumu lakini lazima tushikamane zaidi,” alisema.
Baada ya mchezo dhidi ya Yanga kumalizika, Mwijage alisema sasa nguvu zao zote zinaelekezwa kwenye michezo ijayo dhidi ya timu ambazo zipo kwenye kiwango sawa na KMC.
Alisema mechi hizo ndiyo zitakuwa muhimu zaidi kwao katika harakati za kusaka pointi za kuiokoa timu hiyo.
“Sasa tunaangalia mechi zinazokuja. Tunahitaji kupata kitu kwenye michezo dhidi ya timu zenye levo yetu ili kuinusuru timu,” alisema Mwijage.
KMC imekuwa ikipambana kutoka kwenye nafasi ngumu za msimamo huku kila pointi ikiwa na umuhimu mkubwa katika hatua za mwisho za msimu huu wa Ligi Kuu Bara.