NORMANDY, UFARANSA: SAMAGOAL. Nahodha wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta anayeichezea Le Havre ya Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), leo anatarajiwa kuwa uwanjani kukabiliana na Marseille ya nyota wa kimataifa wa Ebland, Mason Greenwood.
Hadi wiki tatu zilizopita, Greenwood alikuwa anaongoza katika msimamo wa wafungaji bora wa michuano hiyo akiwa na mabao 15 kabla ya kupitiwa na Joao Panichelli wa Strasbourg mwenye 16 kisha wote wakashushwa na Esteban Lepaul anayeongoza kwa sasa na mabao yake 18.
Hata hivyo, Samatta ambaye mwaka huu ametimiza miaka 10 akicheza Ulaya katika timu mbalimbali, amekuwa nyota muhimu katika kikosi cha Le Havre akitoa mchango ulioiwezesha kung’ang’ania katika nafasi ya 14 kati ya timu 18 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Nahodha huyo wa Stars hivi karibuni alishinda tuzo ya nyota bora wa mwezi katika kikosi chake kutokana na ufanisi aliouonyesha wiki za karibuni.
Kikosi chake kinachotumia Uwanja wa Stade Oceane kitakuwa mwenyeji wa mchezo wa Ligue 1 wa raundi ya 33 katika mechi yenye umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili, ambapo wenyeji wanapigania kubaki ligi kuu, huku wageni wakisaka kuendelea kubaki kwenye nafasi za kufuzu mashindano ya klabu Ulaya msimu ujao.
Chini ya kocha Didier Digard, Havre wanashika nafasi ya 14 wakiwa na pointi 32 wakiwa ‘wafalme wa sare’ tano mfululizo, ikiwemo ya bao 1-1 dhidi ya Lille katika mchezo wa mwisho.
Licha ya kutopoteza katika michezo hiyo, Le Havre hawajaonja ushindi katika raundi 10 zilizopita, lakini Digard amejenga mfumo mgumu wa ulinzi unaowasaidia kupata pointi, lakini ukosefu wa ubunifu wa kushambulia bado ni udhaifu wao mkubwa.
Wakiwa nyumbani, Sky Blues huwa wagumu kufungika, na lengo lao katika mchezo huo litakuwa kupunguza kasi ya mchezo na kusubiri Marseille wafanye makosa ili wayatumie kupata alama.
Kwa upande wao, Marseille wanapitia kipindi kigumu kwani baada ya kipigo kizito cha 0-3 dhidi ya Nantes katika raundi iliyopita, kikosi hicho cha Habib Beye kilishuka hadi nafasi ya saba kikiwa na pointi 53 kabla ya mecvji nyingine zilizopigwa jana.
Kwa sasa kikiwa nje ya nafasi za kufuzu Ulaya, hakina nafasi ya kufanya makosa tena. Tatizo kubwa ni kiwango kibovu cha ugenini, ambapo Marseille wamepoteza mechi tatu mfululizo za Ligue 1.
Hata hivyo, kwa ubora wa kikosi, wageni wanaonekana kuwa bora zaidi na macho mengi yatakuwa kwa Greenwood ambaye yupo kwenye tatu bora ya wafungaji wa ligi akiwa na mabao 15.
Kimbinu, Le Havre wanatarajiwa kucheza kwa kujilinda zaidi wakiwa na mabeki watano nyuma, huku Marseille watatawala umiliki wa mpira na kushambulia kupitia pembeni, ambapo ubunifu wa Greenwood unaweza kuwa silaha muhimu ya kuvunja safu ya ulinzi ya wenyeji.
Takwimu zinaonyesha kwamba Marseille wameshinda mechi tano zilizopita dhidi ya Havre kwa jumla ya mabao 19-5. Katika Ligue 1 Le Havre wametoka sare michezo mitano mfululizo na hawajashinda katika michezo 10 iliyopita, huku
Marseille wakishinda mchezo mmoja kati ya sita iliyopita huku wakipoteza mara nne.