Habari za michezo
IVORY COAST INAVYOKABILIWA NA MTIHANI KUVUNJA REKODI
Vardo
May 10, 2026
10:01 am
YAMOUSSOUKRO, IVORY COAST: ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika kwa mara ya kwanza katika mataifa matatu ya Marekani, Canada na Mexico, macho ya mashabiki wengi yameanza kutazama timu zitakazoshangaza mataifa makubwa ya Ulaya na Amerika Kusini.
Bara la Afrika litakuwa na wawakilishi wengi zaidi (10) katika historia ya mashindano hayo kufuatia kuongezwa kwa idadi ya timu zinazoshiriki, jambo ambalo limeongeza matumaini kwa mataifa mengi ya Afrika kuonyesha uwezo wao katika michuano hiyo mikubwa zaidi.
Miongoni mwa timu zinazotajwa kubeba matumaini ya wengi ni Ivory Coast, maarufu kama Les Elephants (Tembo), taifa ambalo kwa miaka mingi limekuwa likiheshimika kwa kuzalisha wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi bora zaidi duniani.
Kwa sasa, Ivory Coast wanaingia katika mashindano hayo wakiwa na kizazi kipya cha nyota kama Amad Diallo anayekipiga Manchester United, Seko Fofana wa FC Porto, Ibrahim Sangare wa Nottingham Forest pamoja na Nicolas Pepe anayekipiga Villarreal ya Hispania.
Lakini nyuma ya kizazi hiki kipya kuna historia ndefu ya mafanikio, majonzi, matumaini na mapambano ambayo yameifanya Ivory Coast kuwa moja ya mataifa yenye hadhi kubwa zaidi katika soka la Afrika.
MWANZO ILIVYOKUWA
Ivory Coast ilianza kushiriki soka la kimataifa rasmi miaka ya mwanzoni mwa 1960, kipindi ambacho mataifa mengi ya Afrika yalikuwa yakitoka katika ukoloni na kujenga mifumo yao ya michezo pamoja na taasisi za kitaifa. Wakati huo, soka lilikuwa sehemu ya kujenga utambulisho wa taifa, kuleta umoja na kuonyesha uwezo wa Waafrika mbele ya dunia.
Katika miaka ya mwanzo, Ivory Coast hawakuwa miongoni mwa mataifa yaliyotajwa sana kama Misri, Ghana au Cameroon, lakini walikuwa wakijenga msingi wa timu yenye ushindani mkubwa. Polepole wakaanza kuonyesha dalili za ukuaji mkubwa katika mashindano ya Mataifa ya Afrika.
Katika AFCON 1965, Ivory Coast walimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuonyesha ushindani dhidi ya mataifa yenye uzoefu mkubwa zaidi. Miaka mitatu baadaye, mwaka 1968, walirudia mafanikio hayo kwa kushika nafasi ya tatu tena, jambo lililoonyesha wazi kuwa taifa hilo lilikuwa linaanza kujenga nguvu mpya katika soka la Afrika.
Mwaka 1970 waliendelea kuthibitisha ushindani wao baada ya kumaliza katika nafasi ya nne. Hata kama hawakuwa wamefika kileleni, walikuwa wameanza kutengeneza heshima kubwa kutokana na uwezo wao.
UBABE ULIPOANZIA
Baada ya miaka mingi ya kusubiri, hatimaye ilifikia kilele mwaka 1992 wakati Ivory Coast walipoandika historia kubwa zaidi kwa kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa AFCON. Mashindano hayo yaliyofanyika nchini Senegal yaliwakutanisha Ivory Coast na Ghana katika mchezo wa fainali. Ndani ya dakika 120 za mchezo huo hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, hali iliyopelekea mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penalti.
Kilichofuata kilikuwa moja ya matukio ya kihistoria zaidi katika soka la Afrika. Ivory Coast waliibuka washindi kwa penalti 11-10 baada ya mfululizo mrefu wa mikwaju iliyowafanya mashabiki kushuhudia moja ya fainali ngumu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya AFCON.
Ushindi huo uliibadilisha kabisa hadhi ya Ivory Coast katika soka la Afrika. Kuanzia hapo hawakuonekana tena kama timu ya kawaida ya ushindani, bali kama moja ya mataifa makubwa yenye uwezo wa kushinda mataji makubwa. Baada ya ubingwa huo, taifa hilo lilianza kuvutia zaidi vipaji vya soka, uwekezaji katika maendeleo ya vijana ukaongezeka, na matumaini ya kuwa nguvu ya kudumu katika soka la Afrika yakaanza kuota mizizi.
KIZAZI CHA DHAHABU
Hakuna sehemu muhimu katika historia ya Ivory Coast inayoweza kutajwa bila kuzungumzia kizazi cha dhahabu kilichoongozwa na Didier Drogba. Nyota huyo hakuwa mshambuliaji wa kawaida, alikuwa nembo ya taifa, sauti ya mashabiki na sura ya mafanikio ya soka la Ivory Coast duniani. Akiwa na nguvu, uwezo mkubwa wa kufunga mabao pamoja na uongozi ndani na nje ya uwanja, Drogba alibeba matumaini ya taifa hilo. Pembeni yake walikuwepo mastaa wengine waliotengeneza moja ya vikosi bora kabisa kuwahi kutokea Afrika kama Yaya Toure, Kolo Toure, Salomon Kalou, Emmanuel Eboue, Didier Zokora pamoja na Gervinho.
Hiki ndicho kizazi kilichofanikiwa kuipeleka Ivory Coast katika fainali za Kombe la Dunia 2006 kwa mara ya kwanza katika historia yao. Kufuzu huko kulikuwa hatua kubwa sana kwa taifa hilo na kulionyesha kuwa lilikuwa limeingia rasmi katika ramani ya soka la dunia.
Katika Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani, Ivory Coast waliwekwa kundi moja na mataifa makubwa kama Argentina na Uholanzi. Licha ya kuonyesha kiwango kizuri na ushindani mkubwa, walishindwa kuvuka hatua ya makundi. Hata hivyo, timu hiyo iliendelea kubaki kuwa tishio. Walifuzu tena kwa fainali za mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na baadaye mwaka 2014 nchini Brazil.
Katika mashindano yote hayo, Ivory Coast walikuwa na kikosi chenye vipaji vikubwa, lakini walikumbana na changamoto za makundi magumu pamoja na presha kubwa ya mashindano. Mara nyingi walionekana kuwa na uwezo wa kufika mbali zaidi, lakini walikosa bahati au umakini katika mechi muhimu.
Licha ya kutofika robo fainali wala hatua ya mtoano, kizazi hicho kiliacha alama kubwa katika soka la Afrika. Kiliifanya Ivory Coast kuwa taifa linaloheshimiwa duniani na kufungua milango kwa wachezaji wengi wa Afrika kwenda kucheza katika ligi kubwa za Ulaya.
MAUMIVU YA MIAKA MINGI
Baada ya miaka mingi ya kukaribia mafanikio bila kuyafikia, Ivory Coast walirejea tena kileleni mwa soka la Afrika mwaka 2015 kwa kutwaa ubingwa wao wa pili wa AFCON. Fainali dhidi ya Ghana ilikuwa ya kihistoria na yenye hekaheka kubwa. Kama ilivyokuwa mwaka 1992, mchezo huo uliamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya sare tasa ndani ya dakika 120.
Ivory Coast waliibuka washindi kwa penalti 9-8 katika mchezo uliokuwa na presha kubwa. Ushindi huo ulikuwa na maana kubwa kwa sababu ulihitimisha miaka mingi ya kukosa mataji licha ya kuwa na kizazi bora cha wachezaji. Kwa mashabiki wengi wa Ivory Coast, ubingwa huo ulikuwa zawadi kwa Didier Drogba na kizazi chake kilichobeba matumaini ya taifa kwa muda mrefu.
KUZALIWA KWA KIZAZI KIPYA
Miaka ya hivi karibuni imeleta hadithi mpya kabisa ya matumaini kwa taifa hilo. Wakiwa wenyeji wa AFCON 2023, wengi waliamini Ivory Coast walikuwa na nafasi nzuri ya kufanya vizuri mbele ya mashabiki wao. Hata hivyo, mwanzo wa mashindano haukuwa mzuri. Timu ilikumbana na matokeo mabaya yaliyowakatisha tamaa mashabiki wengi huku presha ikiongezeka kila siku.
Katika mazingira hayo magumu, uamuzi wa kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi ulimpa nafasi Emerse Fae kuiongoza timu katikati ya mashindano. Kuanzia hapo, kila kitu kilibadilika. Ivory Coast walionyesha mabadiliko makubwa pamoja na nidhamu ya hali ya juu. Waliwang’oa mabingwa watetezi Senegal katika mchezo uliokuwa mgumu, kabla ya kupambana dhidi ya Mali na baadaye DR Congo.
Katika fainali, walikutana na Nigeria na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Ushindi huo ulikuwa ujumbe tosha kuwa Ivory Coast wamezaliwa upya na wako tayari kurejea katika kiwango cha juu cha ushindani.
KIKOSI CHA SASA
Ivory Coast ya sasa inaonekana kuwa moja ya vikosi vilivyokamilika zaidi Afrika. Nahodha Franck Kessie ameendelea kuwa moyo wa timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kucheza kwa utulivu, kupora mipira pamoja na kusaidia mashambulizi. Katikati ya uwanja, uwepo wa Ibrahim Sangare na Seko Fofana umeongeza nguvu kubwa na ubunifu wa kushambulia.
Safu ya ushambuliaji nayo imejaa kasi, ufundi na uwezo wa kubadili matokeo kwa haraka kupitia Amad Diallo, Simon Adingra pamoja na Nicolas Pepe. Katika eneo la ulinzi, vijana kama Odilon Kossounou na Evan Ndicka wameongeza uimara mkubwa na kuifanya timu hiyo kuwa ngumu kufungika. Kinachowafanya Ivory Coast kuwa hatari zaidi ni kwamba wana uwezo wa kucheza kwa kasi, kushambulia kwa kushtukiza na pia kumiliki mpira kwa muda mrefu pale inapohitajika.
WALIVYOFUZU KOMBE LA DUNIA
Katika hatua za kufuzu kuelekea Kombe la Dunia 2026, Ivory Coast, wakiwa Kundi F, walionyesha kiwango bora kilichowafanya watazamwe kama moja ya timu bora kutoka Afrika. Walicheza kwa nidhamu kubwa, wakifunga mabao 25 huku wakionyesha uimara mkubwa wa safu ya ulinzi kwa kutoruhusu bao hata moja. Kocha Emerse Fae ameonekana kuijenga timu yenye kujiamini, umoja pamoja na uwezo wa kubadilika kulingana na aina ya mpinzani anayekutana naye. Katika mechi nyingi za kufuzu, Ivory Coast, ambao waliongoza kundi hilo wakiwa na pointi 26 kufuatia kushinda mechi nane na kutoa sare mbili, walionekana kuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo, jambo lililoonyesha kukomaa kwa kizazi hiki kipya cha wachezaji.
Mashabiki wengi wa Afrika wanaamini kuwa hii inaweza kuwa timu bora zaidi ya Ivory Coast tangu kizazi cha Drogba na wenzake.
KUVUNJA HISTORIA
Kwa miaka mingi, ndoto kubwa ya Ivory Coast imekuwa ni kuvuka hatua ya makundi ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yao. Mwaka huu wanaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya hivyo kutokana na ubora wa kikosi chao. Wababe hao wapo Kundi E pamoja na Ujerumani, Curacao na Ecuador.