Habari za michezo

TANZANITE QUEENS MZIGONI LEO DHIDI YA CAMEROON

Vardo May 10, 2026 10:04 am

HAKUNA namna, ndivyo unavyoweza kusema kwa Timu ya Taifa ya Wasichana U-20, Tanzanite Queens, inayohitaji ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cameroon ili kufuzu kucheza Kombe la Dunia nchini Poland, mechi itakayopigwa saa 10:30 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Hii ni raundi ya nne na ya mwisho ya kutafuta timu nne kutoka Afrika zitakazowakilisha bara hilo kwenye fainali hizo zitakazopigwa kuanzia Septemba 5 hadi 27, mwaka huu. Ni mechi ya marudiano baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini kwenye Uwanja wa Ahmadou Ahidjo, Yaounde, ambapo Tanzania ilikubali kichapo cha mabao 3-1, hivyo Tanzanite ina kibarua cha kushinda mabao 2-0 ili kufuzu moja kwa moja.

Tanzanite inacheza na Cameroon ambayo imekuwa na muendelezo mzuri kwenye hatua hizi. Timu hiyo ilianzia hatua ya pili kama ilivyo kwa Tanzanite. Iliitoa Niger kwa jumla ya mabao 18-0 baada ya kuichapa 9-0 ugenini na nyumbani, kisha katika raundi ya tatu ikaitoa Botswana kwa jumla ya mabao 5-1.

Kwa sasa kwenye raundi hii ya nne tayari imeifunga Tanzanite mabao 3-1. Hivyo, Cameroon ni timu hatari kwenye hatua hizi za mtoano na Tanzanite inapaswa kuwa makini wakati wa kushambulia na hata wakati wa kuzuia, kwani asilimia kubwa ya wachezaji wa Cameroon wako fiti.

Kwenye mechi iliyopita, Tanzanite ilipata bao la mapema kupitia kwa Winifrida Gerald, lakini hawakuwa watulivu hasa kwenye eneo la kiungo wa ukabaji. Timu ilikuwa na haraka ya kushambulia, jambo lililoipa faida Cameroon kusawazisha kabla ya kuongeza mabao mengine.

Cameroon kwenye mechi iliyopita walionekana kuwa na madhaifu pembeni, hivyo Tanzanite inaweza kutumia mabeki wa pembeni kushambulia, lakini isiwasogeze wote kwa pamoja kwani timu hiyo iko vizuri kwenye mashambulizi ya kushtukiza.

Hii si mara ya kwanza Tanzania kukutana na Cameroon, kwani mwaka 2022 Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya miaka 17 ilifuzu Kombe la Dunia la Wanawake U-17 lililofanyika India na kuishia robo fainali. Katika harakati za kufuzu mashindano hayo, Tanzania iliiondosha Cameroon kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya kushinda 4-1 ugenini na baadaye 1-0 nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Tanzanite ina nyota wa kuamua mechi kama winga Hasnath Ubamba anayekipiga FC Masar ya Misri, ambaye alikosekana kwenye mechi iliyopita, lakini kurejea kwake kunaweza kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho.

Nyota mwingine wa kuamua mechi hiyo kwenye eneo la ushambuliaji ni Winifrida Gerald ambaye ameonyesha kiwango bora akiwa tayari amefunga mabao manne hadi sasa.

Mwingine ni Alia Fikirini ambaye kocha Bakari Shime akimtumia vizuri anaweza kuwa na faida kubwa kutokana na kasi yake na uwezo wa kuwachomoka mabeki wa timu pinzani.

Kocha wa timu hiyo, Shime alisema: “Tumekuwa na maandalizi mazuri hapa Zanzibar na tunaamini leo itakuwa mechi ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu, lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na kufuzu, ingawa si rahisi.”

IVORY COAST INAVYOKABILIWA NA MTIHANI KUVUNJA REKODI SABABU IVORY COAST KUCHAGUA PHILADELPHIA MAANDALIZI YA KOMBE LA DUNIA