Habari za michezo

SABABU IVORY COAST KUCHAGUA PHILADELPHIA MAANDALIZI YA KOMBE LA DUNIA

Vardo May 10, 2026 10:10 am

PHILADELPHIA, MAREKANI: WAKATI mataifa mengi yanayojiandaa na Kombe la Dunia 2026 yakisaka mazingira bora ya maandalizi, Ivory Coast wameonekana kufanya maamuzi ya kimkakati kwa kuichagua Philadelphia kuwa moja ya vituo vyao muhimu kuelekea mashindano hayo makubwa yatakayofanyika Amerika Kaskazini.

Taarifa kutoka Marekani zinaeleza kuwa ‘Les Elephants’ wamevutiwa zaidi na miundombinu ya kisasa ya Philadelphia Union, hususani kituo cha mazoezi cha Subaru Park pamoja na WSFS Bank Sportsplex kilichopo Chester, Pennsylvania. Eneo hilo lina viwanja vya kisasa, gym kubwa pamoja na mazingira tulivu yanayofaa kwa maandalizi ya muda mrefu.

Moja ya sababu kubwa iliyowafanya Ivory Coast kuichagua Philadelphia ni ubora wa vifaa vya mazoezi vinavyotumiwa na Philadelphia Union kwenye Ligi Kuu Marekani (MLS). Kambi hiyo inaaminika kuwa miongoni mwa vituo bora zaidi vya soka nchini Marekani kwa sasa kutokana na teknolojia zake za kisasa za matibabu ikiwemo kurejesha utimamu wa wachezaji ‘recovery’.

Pia, Philadelphia imeonekana kuwa sehemu rahisi kwa usafiri kuelekea miji mbalimbali itakayokuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Dunia. Kutoka eneo hilo, timu inaweza kusafiri kwa urahisi kwenda New York, Boston, Atlanta na hata Toronto bila kutumia muda mwingi angani, jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza uchovu wa wachezaji wakati wa mashindano.

Ripoti kutoka vyombo vya habari Marekani zinaeleza kuwa hali ya hewa ya Philadelphia pia imevutia viongozi wa Ivory Coast. Ingawa si sawa kabisa na Afrika Magharibi, mazingira yake wakati wa kiangazi yanaaminika kuwa rafiki kwa maandalizi ya timu.

Kocha Emerse Fae anadaiwa kutaka eneo litakalowapa wachezaji utulivu wa kutosha mbali na presha kubwa za kisoka zinazoweza kujitokeza kwenye miji yenye msongamano mkubwa kama New York au Los Angeles.

Sababu nyingine inayotajwa ni usalama pamoja na faragha ya kikosi. Viongozi wa Ivory Coast wanaamini eneo la Chester linaweza kuwapa nafasi ya kufanya mazoezi kwa utulivu bila usumbufu mkubwa wa mashabiki na vyombo vya habari, tofauti na miji mingine yenye kelele nyingi za mashindano.

Katika mipango yao ya ndani, Ivory Coast wanaamini kuwa kuweka kambi karibu na viwanja vya kisasa vya Marekani kutawasaidia wachezaji kuzoea mazingira ya mashindano mapema.

Pia kuna taarifa kuwa viongozi wa Philadelphia Union walitoa ushirikiano mkubwa kwa Shirikisho la Soka Ivory Coast tangu hatua za mwanzo za mazungumzo. Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mpango wa kuifanya Philadelphia kuwa maskani yao ya muda wakati wa Kombe la Dunia.

Mashabiki wa Ivory Coast wanaoishi Marekani wanatajwa kuwa sababu nyingine muhimu. Philadelphia na maeneo ya karibu yana jamii kubwa ya Waafrika Magharibi, jambo ambalo linaweza kuipa timu sapoti kubwa wakati wa maandalizi na hata siku za mechi.

Kwa upande wa kiufundi, benchi la ufundi la Ivory Coast linaamini mazingira ya Philadelphia yanaweza kusaidia kuijenga timu yenye mshikamano mkubwa kabla ya kuingia kwenye presha za Kombe la Dunia.

HII NDO PHILADELPHIA

Philadelphia yenye zaidi ya wakazi milioni 1.5 ipo upande wa mashariki wa Marekani ndani ya jimbo la Pennsylvania na ni moja ya miji mikubwa na yenye historia ndefu zaidi nchini humo.  Mji huo umezungukwa na mito mikubwa ya Delaware River na Schuylkill River ambayo huupa mandhari ya kuvutia pamoja na hali ya hewa yenye utulivu katika baadhi ya maeneo.

Kuna bustani kubwa, maeneo mengi ya kijani pamoja na sehemu za wazi zinazoufanya mji huo kuwa kivutio kwa wakazi na watalii kutoka mataifa mbalimbali. Kwa upande wa michezo, Philadelphia ni moja ya miji yenye utamaduni mkubwa wa michezo Marekani.

Wakazi wake wana mapenzi makubwa na soka kupitia klabu ya Philadelphia Union lakini pia michezo mingine kama basketball, baseball na American football ina mashabiki wengi sana.

Kwa upande wa usafiri, Philadelphia ina mfumo wa kisasa unaorahisisha watu kusafiri ndani na nje ya mji huo. Kuna treni za kisasa, mabasi, barabara kubwa pamoja na uwanja wa ndege wa Philadelphia International Airport ambao ni miongoni mwa viwanja vikubwa vya ndege Marekani.

TANZANITE QUEENS MZIGONI LEO DHIDI YA CAMEROON