Habari za michezo

MAFANIKIO AFRIKA YAMETUBEBA, SIO KUIFUNGA PAMBA, AHMEDY

Vardo May 10, 2026 8:26 pm

BAADA ya kutwaa tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka 2025 iliyotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), uongozi wa Simba SC umeonyesha kujiamini zaidi ukieleza kuwa mafanikio hayo hayajatokana na kushinda mechi za kawaida za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya timu kama Singida Black Stars au Pamba Jiji FC, bali yametokana na ubora wao katika michuano ya kimataifa.

Usiku wa tuzo za BMT uliofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, uliendelea kuwa wa kihistoria kwa Simba baada ya kutangazwa rasmi kuwa Klabu Bora ya Mwaka 2025 mbele ya wadau mbalimbali wa michezo nchini.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mafanikio hayo yametokana na mwenendo mzuri wa klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa, hususan kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Ahmed amesema baadhi ya watu hawapaswi kushangazwa na Simba kushinda tuzo hiyo kwa kuwa vigezo vya BMT vinazingatia mafanikio ya kimataifa, tofauti na matokeo ya ndani pekee.

Amesisitiza kuwa Simba imeonyesha kiwango kikubwa Afrika, jambo lililowapa nafasi ya kutambuliwa kama klabu bora nchini.

“Msiumie wala msichanganyikiwe na tuzo hii. Kwa mujibu wa BMT, tuzo hizi zinatolewa kwa klabu yenye mafanikio ya kimataifa. Msimu uliopita sisi tulicheza fainali ya Afrika wakati wengine waliishia hatua ya makundi. Hivyo msishangae kuona Simba ikitwaa tuzo hii,” amesema Ahmed.

Katika kinyang’anyiro hicho, Simba iliibuka mshindi mbele ya timu ya mpira wa kikapu ya Dar City, huku mafanikio yao ya mwaka 2025 yakitajwa kujumuisha kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na kimataifa pamoja na kutinga fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.

Tuzo hiyo imeonekana kuwa matokeo ya mshikamano mkubwa kati ya wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa Simba, ambao wameendelea kuwa nguvu muhimu katika safari ya mafanikio ya klabu hiyo ya Msimbazi.

DODOMA JIJI WAPEWE TAHADHARI, MPIGA SIMU WA YANGA AMERUDI RUSHINE AWEKA WAZI KILICHOIPA SIMBA NGUVU MSIMU HUU