Habari za michezo

RUSHINE AWEKA WAZI KILICHOIPA SIMBA NGUVU MSIMU HUU

Vardo May 10, 2026 8:33 pm

BEKI wa Simba SC, Rushine De Reuck amesema ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni mkubwa na wenye presha kubwa, sawa na ligi nyingine zenye ushindani mkali barani Afrika.

Hata hivyo, amesema jambo linalowapa nguvu wachezaji wa Simba ni hamasa ya kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri kila inaposhuka dimbani.

Rushine amesema tangu alipojiunga na Simba ameanza kuzoea mazingira ya soka la Tanzania na anaendelea kufurahia maisha ya soka ndani ya klabu hiyo.

Ameeleza kuwa anafanya kazi kwa bidii kila siku ili kuhakikisha anatoa mchango mkubwa kwa timu katika kufikia malengo yake ya msimu huu.

Beki huyo ameweka wazi kuwa anaelewa ukubwa wa Simba pamoja na matarajio makubwa ya mashabiki wake, jambo ambalo linamfanya kuongeza juhudi zaidi kila anapopata nafasi ya kucheza akiwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

“Ligi ni ngumu, lakini hali kama hii nimeiwahi Afrika Kusini. Kitu muhimu ni kucheza vizuri na kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri,” amesema Rushine akizungumzia ushindani wa Ligi Kuu Bara.

Nyota huyo amesema anafurahishwa na namna kiwango chake kinavyoendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda.

Amebainisha kuwa ataendelea kutumia uwezo wake wote kuhakikisha analisaidia vyema eneo la ulinzi la Simba katika michezo iliyosalia msimu huu.

“Siyo siri kuwa Simba haijashinda ligi kwa muda mrefu, lakini sisi tunaendelea kupambana kadri ya uwezo wetu. Unajua mpira una mambo mengi na chochote kinaweza kutokea, hivyo bado tuna matumaini makubwa,” amesema Rushine.

MAFANIKIO AFRIKA YAMETUBEBA, SIO KUIFUNGA PAMBA, AHMEDY USIPOFANYA UAMUZI SASA, HELIKOPTA YA USHINDI ITAONDOKA