KIUNGO wa Yanga Princess, Maimuna Hamis ‘Mynaco’ amesema ushindani uliopo katika kikosi hicho ndiyo siri inayowafanya wachezaji wote kuongeza kiwango na kuwania nafasi kila wanapocheza.
Akizungumza na Soka la Bongo, Mynaco amesema Yanga Princess hakuna mchezaji mwenye nafasi ya kudumu kutokana na ushindani mkubwa uliopo hasa eneo la kiungo, jambo linalowafanya wote kujituma zaidi mazoezini na hata wanapokuwa uwanjani.
“Kwenye timu mkiwa wachezaji wawili kwenye nafasi moja nafikiri inaleta kitu kizuri, ndiyo maana Yanga kila mchezaji anapata nafasi kutokana na ushindani wa kila mmoja,” amesema Mynaco.
Kiungo huyo aliongeza benchi la ufundi limekuwa likitoa nafasi kwa mchezaji anayepambana zaidi mazoezini na kuonyesha uwezo mkubwa pindi anapopewa nafasi ya kucheza.
“Inamaanisha kujituma kwako na kupambana kocha anaona na atakupa nafasi tu kwenye mechi, ukipewa nafasi na kuionesha kweli kweli,” amesema.
Yanga ina idadi kubwa ya viungo wa kati na wakabaji wenye ushindani mkubwa akiwemo Agnes Pallangyo, Ritticia Nabbosa, Mynaco, Irene Kisisa, Lydia Akoth pamoja na Adebis Oluwa.
Kocha wa timu hiyo, Edna Lema amekuwa akifanya mabadiliko ya kila mechi kuanza na kiungo tofauti kulingana na mahitaji ya mechi husika.
“Kwanza tunashukuru tumetengeneza timu, ndiyo maana unaona kila mechi tunaanza na kiungo mwingine na wakati mwingine naanza na chipukizi ili kuwajengea kujiamini zaidi,” amesema Lema.