HALI ya sintofahamu imeibuka kwa wachezaji nyota wa kikosi cha Azam FC, baada ya kudaiwa kukumbwa na tatizo la kupumua kwa shida, lililotokea tangu mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya TRA United, iliyopigwa Mei 8, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Azam FC ilichapwa mabao 4-1, ikiwa ni kichapo cha kwanza kwa timu hiyo msimu huu Ligi Kuu Bara, kisha baada ya hapo ndipo ikaibuka hali ya sintofahamu.
Sintofahamu iliyoibuka ni baada ya kudaiwa baadhi ya wachezaji wa Azam kukutana na hali mbaya ya hewa katika mechi hiyo, iliyosababisha kushindwa kupumua vizuri, huku vyanzo vikieleza uchunguzi zaidi unaendelea kujua ukweli wa tatizo hilo.
Miongoni mwa wachezaji wanaodaiwa wako katika hali mbaya ni Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ashrafu Kibeku, Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo ambao bado afya zao hazijaimarika, huku uchunguzi ukiendelea katika Hospitali ya Saifee, Dar es Salaam.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti, uchunguzi wa kina unaendelea kujua tatizo na chanzo chake, japo ni jambo lililowashtua viongozi wa kikosi hicho kutokana na mazingira ya kutofurahisha waliyokutana nayo jijini Arusha.
“Kwa sababu uchunguzi bado haujakamilika ni vyema tukawa na subira ili tupate ukweli wa kilichotokea, ila ni kweli kabla na baada ya mechi yetu na TRA United kila kitu tuliona kilibadilika ghafla kwa wachezaji wetu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya dakika 45 za kwanza, ndipo hali ilibadilika kidogo kidogo kwa wachezaji na kuathiri kwa ujumla utendaji wao wa kazi uwanjani, ila waliona kawaida kabla ya kushtushwa na maendelezo ya mchezaji mmoja mmoja.
“Suala la kula chakula ambacho labda hakikuwa vizuri siwezi kulizungumzia kwa sasa kwa sababu halina ushahidi wa moja kwa moja, uongozi wa juu utakuwa na nafasi ya kutoa ufafanuzi ikiona inafaa,” kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti liliwatafuta viongozi wa Azam FC kwa njia ya simu akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa klabu hiyo, Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’ na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Zakaria Thabit ‘Zaka Zakazi’ lakini hawakupatikana kwa ajili ya kuzungumzia sakata hilo.