Habari za michezo
MAMBO KIBAO BARCELONA IKITWAA UBINGWA LA LIGA
Vardo
May 11, 2026
6:50 pm
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA wametwaa ubingwa wa 29 wa Ligi Kuu Hispania (La Liga), baada ya kuwafunga wapinzani na watani wao, Real Madrid kupitia mechi ya El Clasico, iliyopigwa juzi, lakini nyuma ya pazia kulikuwa na mambo kibao yaliyotawala kabla na baada ya mchezo huo.
Barca walitawazwa mabingwa kwa kuwafunga Real Madrid mabao 2-0, ikiwa ni saa saba tangu kocha wao, Hans Flick alipopokea taarifa za msiba wa baba yake uliotokea huko Ujerumani.
Lakini, katika hilo Barcelona hawakuruhusu hali yoyote ya mashaka kujitokeza wakifanya kazi waliyoitaka ili kutwaa La Liga msimu wa pili mfululizo katika Uwanja wa Camp Nou.
Mabingwa hao watetezi walihitaji pointi moja ili kuwa mabingwa, lakini mabao ya Marcus Rashford na Ferran Torres ndani ya dakika 18 za kwanza yalitosha kuwapa taji mbele ya watani katika mechi ya uamuazi iliyowakutanisha ikiwa ni miaka 95 tangu Real Madrid walipobeba ubingwa mbele ya Atletico Madrid – wapinzani wao wengine Hispania.
Hii ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kutetea ubingwa wa Hispania tangu ilipofanya hivyo mfululizo katika misimu ya 2017–18 na 2018–19. Hakuna timu nyingine isipokuwa Barcelona iliyofanikiwa kutetea ubingwa Hispania tangu Real Madrid walipofanya hivyo miaka 17 iliyopita.
Kwa ushindi wa ubingwa wa 29, Wakatalunya pia wamekaribia zaidi rekodi ya kitaifa inayoshikiliwa na Real Madrid inayoongoza kwa mataji 36. Kinachoufanya mfululizo wa mafanikio ya La Liga kuwa wa kuvutia zaidi ni kiwango cha mafanikio katika kipindi ambacho klabu imekuwa ikikumbwa na changamoto za kifedha.
Lakini jambo kubwa limekuwa kurejea kwa vipaji vya La Masia vinavyolisha kikosi cha kwanza. Wachezaji 10 kati ya watu 23 wametoka katika mfumo wa vijana, akiwemo Dani Olmo na Eric García, waliowahi kucheza sehemu nyingine kabla ya kurejea wakiwa wakubwa.
Hesabu hiyo hata hivyo haimjumuishi Pedri aliyewasili akiwa na miaka 17 na Ronald Araujo aliyesajiliwa na Barcelona B akiwa na miaka 19.
LIGI YA MABINGWA INAIKWEPA BARCELONA?
Lengo linalofuata la Flick katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa sasa litakuwa kubeba ubingwa wa tatu mfululizo (2026–27), na hilo litamfanya afanane na gwiji wa Camp Nou, Pep Guardiola, aliyebeba mataji matatu La Liga mfululizo katika misimu yake mitatu ya kwanza akiwa kocha (2008–09, 2009–10, 2010–11).
Lakini, Guardiola yupo mbali kwa mataji ya Ligi ya Mabingwa, ambapo mzaliwa huyo wa Barcelona alitwaa ubingwa wa Ulaya katika misimu miwili kati ya mitatu na hapo unapozungumzia 2014–15.
Lakini, Flick aliiongoza Barcelona hadi nusu fainali msimu uliopita, ikitolewa na Inter Milan katika michezo miwili, ingawa waliangukia hatua moja mapema msimu huo baada ya timu yake kuzidiwa na Atletico Madrid katika hatua ya robo fainali.
HISIA ZA MESSI
Wakati Barcelona ikibeba tena ubingwa wa LaLiga, miongoni mwa maelfu ya maoni yaliyojitokeza mitandaoni mojawapo lilikuwa lile la Lionel Messi, gwiji wa zamani wa klabu hiyo.
Pamoja na ujumbe kutoka kwa wachezaji wa zamani wenzake kama Gerard Pique na Luis Suarez, mashabiki na mastaa wa soka duniani, pia ilionekana hisia za nyota huyo wa Argentina zikithibitisha tena kwamba huwa hakosi kuungana na Barcelona katika nyakati zao muhimu zaidi.
Messi hakupoteza muda kuzungumza baada ya filimbi ya mwisho ya El Clasico alipoweka kwenye ‘Instagram story’ iliyosambaa haraka miongoni mwa mashabiki wake.
Katika chapisho hilo, Messi aliweka picha rasmi ya Barcelona iliyokuwa ikiadhimisha ubingwa wa LaLiga, akiambatanisha na ujumbe mfupi: “Campeones, Visca el Barça” akimaanisha ‘Mabingwa, Barcelona daima’ kauli ya kuisifu na kuipa heshima Barcelona aliyoichezea kwa zaidi ya miaka 20 tangu akiwa mdogo.
Licha ya kuwa mbali na Uwanja wa Spotify Camp Nou, Messi anaendelea kufuatilia kila kinachoendelea katika timu ambayo alikuwa mmoja wa wapiga kazi kubwa zaidi katika historia ya soka la klabu hiyo.
Zaidi ya hayo, muda aliouchagua kuposti alichofanya uliweka wazi kuwa alitazama mechi kama shabiki akifurahia ushindi wa Barcelona dhidi ya mpinzani wake wa jadi.
Ujumbe kutoka kwa gwiji huyo wa zamani wa Blaugrana ulionyesha mapenzi makubwa aliyonayo kwa klabu hiyo na mashabiki wake. Ingawa havalii tena jezi hiyo, Messi anaendelea kusherehekea kila mafanikio ya Barca kwa shauku ileile aliyoionyesha katika miaka yake Camp Nou.
MABASI YAHARIBIWA
Mvutano unaozunguka ushindani kati ya Barcelona na Real Madrid uliongezeka kabla ya mchezo kuanza Camp Nou wakati wa kuwasili kwa mabasi ya timu zote ulipogeuka vurugu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, makundi ya mashabiki wenye msimamo mkali wa Barcelona walikusanyika nje ya uwanja kuyapokea mabasi hayo yalipokuwa yakiingia uwanjani.
Kilichoanza kama mazingira ya ubabe wa kabla ya mechi kilivuka mipaka haraka baada ya vitu kurushwa kuelekea kwenye magari ya timu hizo mbili.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya mashabiki walikosea na kulenga basi lao wenyewe la Barcelona wakiamini kwamba lilikuwa limekibeba kikosi cha Real Madrid. Dakika chache baadaye, basi halisi la Real Madrid pia lilishambuliwa, safari hii kwa makusudi, huku vitu vikirushwa moja kwa moja kwenye gari lililokuwa limewabeba wachezaji na benchi la ufundi na kuzua taharuki kwa wachezaji waliokuwa ndani.
Uharibifu wa basi la Real Madrid ulionekana wazi baadaye, huku angalau dirisha moja likivunjika wakati wa tukio hilo. Picha zilizosambaa mitandaoni zilionyesha vioo vilivyovunjika na uharibifu wa nje wa basi hilo baada ya kuwasili uwanjani.
Matukio hayo yalilinganishwa mara moja na yale ya hivi karibuni yaliyohusisha Atletico Madrid walipokwenda Camp Nou kwa ajili ya mechi za Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika matukio hayo, basi la Atletico Madrid pia lilishambuliwa na mashabiki na kupata uharibifu wakati wa kuwasili uwanjani.
Matukio yote yamezua hofu kuhusu tabia za mashabiki na hatua za usalama katika mechi kubwa, ambapo kushambuliwa kwa usafiri wa timu limekuwa suala linaloongezeka katika soka la Ulaya, hasa katika mechi zenye hisia kali. Mamlaka zinatarajiwa kupitia video za usalama na kuchunguza matukio yaliyozunguka mashambulizi hayo.
YAMAL ALIVYOMPIKU RONALDO
Baada ya kuifunga Real Madrid katika El Clasico na kutwaa tena taji la LaLiga, staa wa Barcelona Lamine Yamal amempita mmoja wa mastaa wakubwa zaidi katika historia ya Los Blancos.
Lamine Yamal aliingia kikosi cha kwanza cha Barca 2022 na hajawahi kuacha kupata mafanikio tangu wakati huo, na kwa ubingwa huo, mshambuliaji huyo anajivunia mataji matatu ya ligi akiwa na kikosi cha Blaugrana.
Kwa taji hilo jipya, Yamal anafikisha matatu ya LaLiga (2023, 2025, na 2026), na rasmi akimpita Cristiano Ronaldo, aliyeshinda mataji mawili a (2012 na 2017) katika misimu yake tisa akiwa Real Madrid.
Winga huyo Mhispania alikuwa sehemu muhimu ya kampeni ya Barcelona, ingawa hakucheza mchezo wa mwisho wa msimu kutokana na majeraha, jambo ambalo limezua shaka kuhusu uwepo wake katika fainali za Kombe la Dunia zijazo. Ulinganisho huu unaonyesha ubora ambao mchezaji huyo ameuingiza Barcelona, akiwa mojawapo wa alama kubwa za sasa na baadaye za klabu hiyo ya Catalonia.