Habari za michezo

LIVERPOOL YAITISHA CHELSEA KWA ALONSO

Vardo May 11, 2026 6:38 pm

LONDON, ENGLAND: WANAKABANA koo. Ndiyo, kila timu inataka huduma ya Xabi Alonso kwenda kufundisha vikosi vyao na kinachosubiriwa ni kuona nani mwenye kisu kikali atakayekula nyama.

Matajiri wa London, Chelsea imekuwa ikiifukuzia saini ya kocha huyo ili akapige kazi darajani baada ya kumfuta kazi Kocha Liam Rosenior ambaye alikaa Stamford Bridge kwa siku 106 pekee kabla ya kuondolewa kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo, iliyopoteza mechi tano za mwisho za Ligi Kuu England bila hata kufunga bao.

Awali majina ya Andoni Iraola na Marco Silva yalitajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaofuatiliwa lakini sasa Alonso ameibuka kuwa mmoja wa watu wanaopewa nafasi kubwa ndani ya uongozi wa Chelsea.

Ripoti kutoka England zinaeleza baadhi ya viongozi wa Chelsea tayari wanamwona Alonso kama ‘chaguo la mapema’ la kupewa kazi hiyo kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa kocha wa Bayer Leverkusen.

Wakati huo huo, miamba ya Anfield, Liverpool inamtaka Alonso akarithi

mikoba ya Arne Slot ambaye inaonekana kutokuwa na msimu mzuri.

Vita ipo kwa timu hizo ambazo zinapambana kufuzu michuano ya Ulaya msimu ujao huku Livepool ikiwa nafasi ya nne na Chelsea ya tisa zikiwa zimesaliwa na mechi mbili kila moja.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 aliweka historia Ujerumani baada ya kuiongoza Leverkusen kutwaa ubingwa wa Bundesliga 2024 kwa kiwango kilichovutia timu nyingi Ulaya.

Mafanikio hayo yalimsukuma kupewa nafasi ya kuifundisha Real Madrid, timu aliyowahi kuitumikia akiwa mchezaji lakini mambo yalimwendea kombo na kuachana nayo baada ya miezi saba.

Hata hivyo, Chelsea inaweza kukutana na ushindani mkubwa kutoka Liverpool ambao nao wanatajwa kumfuatilia Alonso huku presha ikiendelea kuongezeka kwa kocha wao wa sasa, Slot na ina faida ya kumnasa kutokana na kuwahi kukipiga Anfield kabla ya kutoa Madrid.

Liverpool imekuwa kwenye msimu mgumu wa kutetea ubingwa huku mashabiki wengi wakionyesha kutoridhishwa na matokeo ya timu hiyo, hali ambayo imeongeza mjadala wa uwezekano wa Alonso kurejea Anfield kama kocha.

NANE KUCHUANA NUSU FAINSALI FA CUP, ZANZIBAR MAMBO KIBAO BARCELONA IKITWAA UBINGWA LA LIGA