Mashindano ya kusaka vipaji ya BSS 2026 Next Level Revolution, yameingia hatua ya 20 bora baada ya kukamilika kwa mchujo uliowakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki.
Washiriki hao wametambulishwa leo Mei 12, 2026 katika ukumbi wa Tabata Studio 1 jijini Dar es Salaam mbele ya wadau wa sanaa, waandishi wa habari pamoja na waandaaji wa shindano hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, mwandaaji wa mashindano hayo, Rita Paulsen amesema washiriki hao tayari wameingia kambini maeneo ya Ndege Beach kwa ajili ya maandalizi ya hatua inayofuata ya mashindano, huku rekodi za studio zikitarajiwa kuanza rasmi katika siku zijazo.
Amesema kati ya washiriki 20 waliofanikiwa kuingia hatua hiyo, Watanzania wako 10, Wakenya watatu, Waganda wawili na Wakongomani watatu, huku kundi moja la kucheza muziki likiwa na washiriki 15.
Rita amesema pia kuna mshiriki mmoja wa vichekesho kutoka Mbeya aliyefanikiwa kuingia katika hatua hiyo.
“Washiriki wa mwaka huu wana vipaji vikubwa sana, hali iliyotufanya kupata wakati mgumu kuchagua nani abaki na nani aondoke. Kila mmoja alikuwa na uwezo wa kipekee, ndiyo maana hata majaji walikaa kwa muda mrefu kujadili majina ya watakaofika top 20, amesema Rita maarufu kama Madam Ritha mbele ya wanahabari na kuongeza:
“Tunaamini kundi hili litatoa ushindani mkubwa sana kwa sababu wengi wao tayari wanauelewa mkubwa wa sanaa wanayoifanya.”
Ameongeza kuwa hatua inayofuata ya mashindano itajikita zaidi katika kuwafahamu washiriki hao kwa undani kupitia wajibu wao utakaoonyesha historia, umri, maeneo wanayotoka pamoja na safari zao za kisanaa kabla ya kuingia BSS.
“Kuanzia kipindi kinachofuata watu wataanza kuona maisha ya washiriki hawa kwa karibu zaidi. Tutakuwa tunaonesha ‘profile’ zao, wanatoka wapi, wana miaka mingapi, wamepitia changamoto gani na ndoto zao ni zipi. Tunataka watazamaji wajue hawa ni watu wa aina gani kabla ya kuanza ushindani rasmi wa jukwaani,” amesema.
Kuhusu kupatikana kwa mshiriki mmoja pekee upande wa uchekeshaji, Madam Rita ameliambia Mwanaspoti kuwa ushindani ulikuwa mkubwa lakini wengi hawakuweza kukidhi viwango vilivyotakiwa na majaji kwa kipengele hicho.
“Watu wengi walijitokeza upande wa uchekeshaji, lakini ukweli ni kwamba kuchekesha si jambo la kubahatisha kama wengine wanavyofikiri. Aidha unachekesha au huchekeshi. Unaweza kusimama jukwaani ukadhani una ‘material’ mazuri lakini watu wakakuangalia tu bila kucheka. Ndiyo maana tulikuwa makini sana katika uchaguzi huu, hasa tukizingatia tunaye Jaji Coy Mzungu ambaye anaelewa vizuri sana upande wa comedy (vichekesho),” amesema.
Ameendelea kusema kuwa lengo la BSS ni kupata vipaji vyenye ubora wa hali ya juu na siyo kuwachukua washiriki kwa kuwaonea huruma, huku akisisitiza kuwa washiriki wa vichekesho wanapaswa kuwa wabunifu kila wanapopanda jukwaani.
“Hatuwezi kumchukua mtu kwa huruma eti kwa sababu amejaribu. Tunataka mtu ambaye kila akipanda jukwaani analeta kitu kipya na kuwafanya watu wacheke kwa nguvu. Comedy inahitaji ubunifu mkubwa kwa sababu watazamaji hawataki kusikia material yaleyale kila siku. Ndiyo maana tumebaki na mmoja ambaye ameonekana kuwa na uwezo wa kuhimili ushindani huo,” amesema Madam Rita.