Habari za michezo

NICOLAS JACKSON ANUKIA KUTUA ITALIA, JUVENTUS YATAJWA

Vardo May 12, 2026 5:49 pm

JUVENTUS  inatajwa kufikiria kutuma ofa ya kumsajili kwa mkopo kwa mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson, katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.

Nyota huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 24 kwa sasa anaitumikia Bayern Munich kwa mkopo, lakini taarifa zinaeleza kuwa hatobaki ndani ya kikosi hicho cha mabingwa wa Bundesliga msimu ujao kwani hawajaridhishwa na kiwango chake.

Juventus inaonekana kutafuta kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji baada ya kutofanya vizuri msimu huu kuanzia michuano ya ndani na kimataifa.

Nicolas mwenyewe amewaambia wawakilishi wake kwamba haitaji tena kuichezea Chelsea, hivyo kwa msimu ujao ni aidha auzwe ama atolewe kwa mkopo wa msimu mmoja.

Mkataba wa sasa wa Jackson na Chelsean unatarajiwa kumalizika mwaka 2033 na akiwa na Bayern msimu huu amecheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao 10.

Chelsea pia haionekani kuwa na mpango wa kuendelea kuwa naye, hivyo ikiwasilishwa ofa kutoka kwa timu inayomhitaji itakuwa tayari kumuuza.

Jarrod Bowen

MSHAMBULIAJI wa West Ham, Jarrod Bowen ameibuka kwenye rada za vigogo wa Ligi Kuu England, Liverpool, Newcastle United na Everton dirisha lijalo la usajili.

Bowen, 29, amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na vigogo hao kutokana na kiwango chake bora akiwa na West Ham United, huku taarifa zikieleza klabu hizo zitaendelea kuwania saini yake hata kama West Ham itaepuka na janga la kushuka daraja mwishoni mwa msimu huu.

Dani Ceballos

REAL Madrid inaweza kulazimika kuuza baadhi ya wachezaji wake kabla ya kufanya usajili mpya dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Kiungo wa kimataifa wa Hispania, Dani Ceballos, 29, ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuondolewa ikiwa mabosi wa Madrid wataamua kupunguza mastaa ili kutengeneza nafasi ya usajili mpya.

Ceballos amekuwa akihusishwa mara kadhaa  kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.

Emiliano Martinez

ASTON Villa imeanza kutafuta mbadala wa kipa wao, Emiliano Martinez anayetarajiwa kuondoka.

Taarifa zinaeleza makipa wawili kutoka Ligue 1 wameibuka kwenye rada za Villa, Robin Risser wa RC Lens pamoja na Guillaume Restes anayekipiga Toulouse.

Makipa hao wote wana umri wa miaka 21 na ni wachezaji wa timu za taifa za  vijana za Ufaransa na wanatajwa kuwa miongoni mwa vipaji vinavyopewa nafasi kubwa ya kuja kung’ara.

Francisco Trincao

KIUNGO mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Francisco Trincao, yupo katika rada za Liverpool na Chelsea  zinazohitaji kumsajili dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.

Nyota huyo, 26, ameendelea kuonyesha kiwango bora akiwa Sporting, jambo lililowafanya Liverpool na Chelsea kuvutiwa naye na kuanza mazungumzo ya kutaka kumsajili. Mkataba wake umanalizika mwaka 2030.

Noah Sadiki

KIUNGO wa kati wa Sunderland, Noah Sadiki ameweka wazi anaweza akaondoka dirisha lijalo.

Sadiki, 21, amekuwa akionyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu licha ya kucheza Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza.

Klabu nyingi ikiwemo Liverpool zimevutiwa naye sana kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaba na kuchezesha timu. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.

Maghnes Akliouche

Liverpool imeendelea kuimarisha mipango yake ya usajili kwa kuelekeza macho kwa winga wa kulia wa AS Monaco, Maghnes Akliouche.

Nyota huyo, 24, anatajwa kuwa na thamani ya Euro 50 milioni ambayo Liverpool ipo tayari kuitoa kwa sababu inaona anaweza kuongeza ubunifu na kasi kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Mbali na Akliouche, Liverpool pia inamfuatilia kwa karibu  kiungo wa kimataifa wa Senegal, Lamine Camara, ambaye pia anakipiga Monaco. Mateus Fernandes

Mateus Fernandes

WEST Ham imesisitiza inahitaji Pauni 84 milioni ili kumuuza kiungo wao, Mateus Fernandes, anayewindwa na vigogo Ulaya.

Kiungo huyo, 21, anatajwa kufuatiliwa na Manchester United pamoja na PSG na sasa zinafanya mazungumzo na wakala wake.

West Ham inaonekana kutokuwa tayari kumwachia kirahisi nyota huyo, lakini haitokuwa na nguvu ya kumzuia ikiwa itashindwa kuendelea kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao.

KABLA YA PAMOJA HUVUTA MZIGO MZITO, YANGA YAKAMILISHA FAINI BSS NEXT REVOLUTION YAFIKIA TOP 20