Mashabiki na wanachama wa klabu ya Yanga wameonyesha jeuri ya fedha baada ya kufanikisha kuchangisha zaidi ya Sh31 milioni kwa ajili ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kufuatia mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba S.C.
Dakika chache baada ya kamati hiyo kutangaza kuwa imeipiga Yanga faini ya Sh30 milioni ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo uliweka picha na namba ya akaunti ambayo mashabiki na wanachama wanaweza kuchangia huku ikinogeshwa na maneno ‘Bili ya Jumba la Maajabu.’
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kupitia ukurasa wa Instagram wa Yanga, mashabiki walifanikiwa kuchangisha jumla ya Sh31,210,840, kiasi kilichovuka faini ya Sh30 milioni iliyotolewa na kamati hiyo. Kampeni hiyo ya uchangishaji ilipata mwitikio mkubwa kupitia akaunti za benki na huduma za fedha kwa simu muda mfupi baada ya adhabu hiyo kutangazwa.
Klabu hiyo ilieleza kuwa Sh24,310,240 zilipatikana kupitia miamala ya benki, huku Sh6,900,300 zikichangwa kupitia huduma za fedha kwa simu. Baada ya kulipa faini hiyo, zaidi ya Sh1 milioni zilibaki kama ziada.
Kamati hiyo iliitoza Yanga faini hiyo kwa kukiuka kanuni za matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo baada ya timu hiyo kugoma kuingia vyumbani na kukaa kwenye nyumba iliyopo jirani na uwanja huo. Mchezo huo wa watani wa jadi ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Hatua nyingine za kinidhamu ilimkumba meneja wa timu ya Yanga, Walter Harison, ambaye alifungiwa michezo mitatu pamoja na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa madai ya kumsukuma kiungo wa Simba, Clatous Chama, wakati wa mvutano uliotokea pembeni mwa uwanja.