Habari za michezo

SOWAH AKACHA MAZOEZI SIMBA LICHA YA KUREJESHWA KIKOSINI

Vardo May 12, 2026 5:28 pm

Mshambuliaji wa Simba SC raia wa Ghana, Jonathan Sowah, bado hajajitokeza kwenye mazoezi ya timu ya vijana (U-20) ya klabu hiyo, licha ya uongozi wa Simba kumrejesha kikosini kwa masharti ya nidhamu.

Mshambuliaji huyo, ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa, alisimamishwa mapema mwaka huu wakati Simba walipokuwa Dodoma wakijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji FC mwezi Februari.

Katika kipindi hicho, Sowah aliamriwa kurejea Dar es Salaam na tangu wakati huo hajawahi kuichezea timu hiyo ya Msimbazi katika mashindano rasmi. Kutokuwepo kwake kulizua uvumi kuhusu mustakabali wake kabla ya uongozi kuamua kumpa nafasi nyingine kwa masharti maalum ya nidhamu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka klabu, Sowah hivi karibuni alifikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya Simba ambapo alikabiliwa na mashitaka kadhaa ya utovu wa nidhamu. Baada ya kuyapitia, kamati ilimkuta na hatia ya baadhi ya tuhuma na ikaamua arudi kujiunga na timu ya vijana U-20 badala ya kurudi moja kwa moja kikosi cha wakubwa.

Mpango huo ulikuwa sehemu ya adhabu na pia njia ya kumfuatilia mchezaji huyo ili kutathmini nidhamu, uwajibikaji na mwenendo wake kabla ya uamuzi wa mwisho kuhusu kurejea kwake timu ya wakubwa.

Hata hivyo, licha ya maelekezo hayo, Sowah bado hajajiunga na mazoezi ya U-20, hali inayozidi kuongeza sintofahamu kuhusu hatima yake ndani ya klabu.

Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally, alithibitisha kuwa mshambuliaji huyo bado hajaanza mazoezi na timu ya vijana na uongozi unaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo.

“Sowah bado hajafika mazoezini na hakuna taarifa rasmi kuhusu hilo. Uongozi unaendelea kufuatilia hali hiyo na utatoa uamuzi wake. Kwa sasa hali ipo kama nilivyoeleza,” alisema Ally.

Kabla ya hatua hiyo ya sasa, Sowah alikuwa amesisitiza hadharani kuwa soka ni kazi yake na bado amejitolea kuitumikia Simba licha ya changamoto za nidhamu zilizogubika msimu wake.

Mshambuliaji huyo bado ana mkataba na Simba, na viongozi wa klabu wanasema mlango bado uko wazi kwa kurejea kwake kikosi cha wakubwa endapo ataonyesha mabadiliko ya nidhamu na kufuata masharti yaliyowekwa na kamati ya nidhamu.

Sowah alijiunga na Simba akiwa na matarajio makubwa kutokana na kiwango chake kizuri nchini Ghana, lakini muda wake klabuni umekuwa ukikumbwa na changamoto za nidhamu pamoja na nafasi chache uwanjani.

Wakati Simba ikiingia katika hatua muhimu ya msimu, klabu hiyo inatarajiwa kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo baada ya kukamilika kwa mchakato wa ufuatiliaji.

MKUD AWAINGIZA WANAJESHIVITANI KABLA YA PAMOJA HUVUTA MZIGO MZITO, YANGA YAKAMILISHA FAINI