Habari za michezo
UMRI UMEENDA, UBORA HAUJAONDOKA KWA CHAMA
Vardo
May 12, 2026
9:15 am
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Ahmed Ally, amewataka wadau wa soka kuangalia mchango mkubwa wa kiungo Clatous Chama ndani ya timu badala ya kujikita kwenye umri wake.
Ahmed amesema kuwa kuongezeka kwa umri wa mchezaji hakumaanishi moja kwa moja kuwa uwezo wake unapungua, bali kinachoweza kupungua ni nguvu za mwili huku akili ya mchezo ikiendelea kuwa bora zaidi.
Ametolea mfano mastaa wa dunia, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, akisema licha ya umri wao kuongezeka bado wanaendelea kufanya vizuri kutokana na uzoefu na uelewa mkubwa wa mchezo.
“Kwa Chama ni hivyo hivyo, ana akili kubwa ya mpira. Inawezekana nguvu zake zisifanane na za akiwa na miaka 25 au 26, lakini uwezo wake wa kufikiri na kusoma mchezo bado upo juu. Kadri anavyozidi kukua, ndivyo anavyozidi kupata maarifa mapya ndani ya mchezo,” amesema Ahmed.
Amesema uzoefu mkubwa alioupata Chama katika maisha yake ya soka ndio unaomfanya kuendelea kuwa mchezaji muhimu ndani ya Simba SC, akieleza kuwa kwa sasa anafanya baadhi ya vitu ambavyo hakuvifanya akiwa na umri mdogo.
“Chama amepitia mengi kwenye mpira na hilo limemjenga zaidi. Kama msemo unavyosema, nyani mzee amekwepa mishale mingi. Amejifunza mambo mengi kupitia uzoefu wake na ndio maana anaendelea kufanya makubwa,” amesema.
Ahmed ameongeza kuwa si sahihi kwa baadhi ya watu kujificha kwenye hoja ya umri na kudai kuwa Chama hafai tena, akisisitiza kuwa Simba itaendelea kumuunga mkono kutokana na mchango mkubwa anaoendelea kutoa kwa klabu hiyo.