Habari za michezo
SIMBA YAJIPANGA KUVUNJA UGUMU WA LAKE TANGANYIKA
Vardo
May 12, 2026
9:20 am
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kikosi hicho kinaelekea Kigoma kikiwa na lengo moja kubwa la kuhakikisha kinarejea na alama tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa Mei 14 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
Ahmed amesema Simba haitakwenda Kigoma kwa matarajio ya miujiza, bali imejipanga kupambana kwa nguvu zote ili kupata ushindi mbele ya Mashujaa ambao wamekuwa wakionyesha ushindani mkubwa wanapocheza katika mazingira yao ya nyumbani.
Amesema mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na ubora wa wapinzani wao, huku akisisitiza kuwa Simba inaipa heshima kubwa Mashujaa pamoja na benchi lao la ufundi linaloongozwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Kwa mujibu wa Ahmed, Julio ni kocha mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania kutokana na historia yake ya kucheza na baadaye kufundisha kwa mafanikio, jambo ambalo linaifanya Simba kuwa makini zaidi kuelekea mchezo huo muhimu.
“Kimsingi maisha yake yote ni mpira, hivyo unapokutana na mwalimu wa namna hiyo lazima ujue mchezo utakuwa mgumu na wa ushindani mkubwa,” amesema Ahmed akizungumzia uwezo wa kocha huyo wa Mashujaa.
Ahmed amesema mara nyingi Simba imekuwa ikipata wakati mgumu inapokutana na Mashujaa katika uwanja wao wa nyumbani, hali inayowalazimu kufanya maandalizi ya kina kuhakikisha safari hii wanapata matokeo mazuri mapema.