Habari za michezo

WAARABU WAMVUTIA WAYA NABI, MAJU YAKE HAYA HAPA

Vardo May 12, 2026 9:25 am

KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameigomea kwa sasa ofa Wydad Casablanca ya Morocco na kuwataka wasubiri hadi mwisho wa msimu ili kurithi mikoba ya Patrice Carteron aliyesitishiwa mkataba wake kutokana na madai ya matokeo yasiyoridhisha.

Taarifa kutoka Morocco zinaeleza Wydad ilianza mazungumzo ya haraka na Nabi baada ya kuvunja mkataba wa Carteron huku jina la kocha huyo likionekana kuwa chaguo la kwanza kutokana na uzoefu wake mkubwa kwenye soka la Afrika.

Hata hivyo, Nabi ameweka wazi kuwa ratiba iliyobaki ya msimu ni ngumu na haitampa muda wa kutosha kuijenga timu kwa mtindo anaoutaka, jambo lililomfanya kuahirisha maamuzi ya kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Afrika.

Kocha huyo anayeheshimika Tanzania hasa na mashabiki wa Yanga, amesema yupo tayari kuichukua Wydad mwishoni mwa msimu wakati wa mapumziko, hatua inayotafsiriwa kuwa mlango bado uko wazi kwa mazungumzo ya baadaye.

Uamuzi huo umeamsha kumbukumbu kwa mashabiki wa Yanga waliowahi kushuhudia mafanikio makubwa chini ya Nabi katika kipindi chake cha siku 786 alizokaa Jangwani.

Nabi alitua Yanga Aprili 2021 na kuibadilisha timu hiyo ndani ya muda mfupi, akiiwezesha kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Bara, mataji mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam pamoja na Ngao za Jamii.

Mbali na mataji hayo, rekodi kubwa iliyompa heshima ilikuwa kuifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2023, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kucheza fainali ya mashindano ya CAF katika historia yake.

Katika kipindi chake cha mafanikio, Nabi aliweka pia rekodi ya kucheza mechi 49 bila kupoteza akiwa Yanga huku akionekana kubadilisha kabisa mfumo na falsafa ya timu hiyo.

Miongoni mwa wachezaji ambao waliendelezwa na Nabi wakati akiwa Tanzania ni pamoja na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alimgeuza kutoka kiungo mkabaji hadi kuwa mmoja wa viungo washambuliaji bora Tanzania.

Pia Nabi aliwahi kuandika historia kwenye dabi dhidi ya Simba ambapo katika mechi nane alizokutana na watani hao, alishinda nne, sare tatu na kupoteza moja pekee.

SIMBA YAJIPANGA KUVUNJA UGUMU WA LAKE TANGANYIKA SINGIDA, JKT, TRA KUPIGANIA NAFSI NNE ZA JUU LIGI KUU