Habari za michezo

KIPIGO HAKITIKISI JESHI LA YANGA, WATOA TAHADHARI KWA WAPINZANI

Vardo May 13, 2026 10:07 pm

BAADA ya kupoteza mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC, uongozi wa Yanga SC umeweka wazi kuwa matokeo hayo hayajawaondolea morali ya kuendelea kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ukisisitiza kuwa kilichotokea ni sehemu ya kawaida ya mchezo wa soka.

Msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe amesema benchi la ufundi tayari limebaini maeneo yaliyokuwa na mapungufu katika mchezo huo, huku hatua mbalimbali zikianza kuchukuliwa ili kuhakikisha makosa hayo hayajirudii katika mechi zijazo.

Kamwe amesema ndani ya kikosi hakuna sababu ya kulaumiana baada ya kupoteza mchezo huo, akieleza kuwa timu ilikuwa kwenye hali nzuri kabla ya mchezo huo na wachezaji wengi walikuwa fiti kwa ajili ya ushindani huo.

Aidha, amesema hata ratiba ya mechi haijawa ngumu kiasi cha kuathiri kiwango cha timu hiyo.

“Hatuna wa kumlaumu kwa matokeo haya kwa sababu wachezaji wengi wamepona na ratiba haijabana sana. Ni mpira, imetokea siku ya kufungwa tukiwa kamili, hakuna aliyepata majeraha,” amesema Kamwe.

Amefafanua kuwa Yanga inaichukulia changamoto hiyo kama sehemu ya kujifunza na kujipanga upya kuelekea michezo inayofuata, huku akisisitiza kuwa tofauti ya pointi kati yao na timu inayowafuata bado inawapa nafasi nzuri ya kuendelea kujiamini katika mbio za ubingwa.

Kamwe ameongeza kuwa kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika kuhakikisha timu inarejea kwenye kiwango chake bora haraka iwezekanavyo, huku akisisitiza kuwa Yanga bado ipo kileleni mwa msimamo wa ligi na itaendelea kupambana hadi mwisho wa msimu ili kuhakikisha inafikia malengo yake ya kutwaa taji.

SIMBA YATAMBA MAKOMBE MAWILI BADO TUNAWEZA KUYABEBA JANGWA HALIJAWAHI KUKOSA UTAJIRI, JIKUSANYIE SEHEMU YAKO MAPEMA