Habari za michezo
SIMBA YATAMBA MAKOMBE MAWILI BADO TUNAWEZA KUYABEBA
Vardo
May 13, 2026
9:58 pm
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kwa sasa nguvu, akili na mipango yote ya klabu hiyo imeelekezwa katika mbio za kusaka mataji mawili makubwa yaliyobaki msimu huu ambayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Ahmed amesema Simba tayari imefanikiwa kutwaa Kombe la Muungano, hivyo sasa lengo kubwa lililobaki ni kuhakikisha timu hiyo inaongeza mataji mengine mawili ili kuhitimisha msimu kwa mafanikio makubwa zaidi.
Ameeleza kuwa ndani ya kikosi hicho bado kuna ari, morali na imani kubwa ya kufanya vizuri katika mechi zilizobaki.
“Kwanza tayari tuna Kombe la Muungano, sasa mbele yetu kuna makombe mawili, Ligi Kuu na Shirikisho. Hapo ndipo akili na nguvu zetu zote zilipo,” amesema Ahmed.
Akizungumzia namna ambavyo Simba imejipanga katika hatua hizi za mwisho wa msimu.
Amesisitiza kuwa Simba bado ina nafasi kubwa ya kutwaa mataji yote mawili kutokana na ubora wa kikosi hicho, uzoefu wa wachezaji pamoja na namna benchi la ufundi linavyoendelea kuisimamia timu katika kipindi hiki chenye ushindani mkubwa.
Ahmed amesema hata kama mambo hayatakwenda kama ambavyo wanatarajia, bado wanaamini Simba haiwezi kuumaliza msimu bila kubeba angalau moja ya mataji hayo mawili.
Kauli hiyo imeonyesha wazi dhamira na presha kubwa waliyojiwekea kuhakikisha mashabiki wao wanapata sababu ya kusherehekea mwishoni mwa msimu.
Akizungumzia Kombe la Shirikisho la CRDB, Ahmed amesema mbio za ubingwa bado ziko wazi kwa timu zote zilizofanikiwa kutinga hatua ya robo fainali, akisisitiza kuwa hakuna klabu yenye uhakika wa kutwaa taji hilo kwa sasa.
Ameongeza kuaa timu ambayo itaonyesha ubora mkubwa katika michezo ya robo fainali, nusu fainali na fainali ndiyo itakayofanikiwa kubeba ubingwa huo.