Habari za michezo
KAMWE AAMINI DUBE ATAIBEBA YANGA KUTETEA UBINGWA
Vardo
May 14, 2026
10:44 am
BAADA ya Yanga SC kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Airtel mjini Singida, msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe amemtetea mshambuliaji Prince Dube kutokana na kushindwa kutumia baadhi ya nafasi alizopata katika mchezo huo.
Kamwe amesema licha ya Dube kutokuwa na bahati ya kufunga, bado ameendelea kuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na namna anavyosaidia kuunganisha safu ya ushambuliaji pamoja na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wengine.
Ameeleza kuwa Yanga ilicheza kwa ushindani mkubwa katika dakika zote za mchezo huo, lakini kushindwa kuzitumia vizuri nafasi za mwisho mbele ya lango ndiko kulikochangia kupoteza alama tatu muhimu dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Kwa mujibu wa Kamwe, nafasi nyingi za mwisho zilikuwa zikimkuta Dube kutokana na nafasi yake ya ushambuliaji, lakini siku hiyo mambo hayakwenda kama walivyotarajia, akisisitiza kuwa hali kama hiyo ni jambo la kawaida ndani ya mchezo wa soka.
“Tunazidi kusimama naye na tunaendelea kumpa moyo. Itakuwa bora na atapata matokeo mazuri zaidi. Bado tunaamini ni mshambuliaji mzuri ambaye anaweza kutufikisha nchi ya ahadi na kutusaidia kutetea ubingwa wetu,” amesema Kamwe.
Licha ya kupoteza mchezo huo, Yanga bado ipo kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku benchi la ufundi pamoja na uongozi wa klabu hiyo vikionesha kuendelea kuwa na imani kubwa kwa kikosi chao katika harakati za kutetea taji msimu huu.