WAZIRI AFICHUA SIRI YA KUILAZIMISHA YANGA SINGIDA
MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji FC, Waziri Junior amesema maelekezo ya kocha wao, Amani Josiah ndiyo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa ushindi walioupata dhidi ya Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Airtel, Singida.
Waziri alisema akiwa benchi, kocha alimpa maelekezo maalumu ya kuangalia mapungufu yaliyokuwa yakionekana kwa wapinzani wao, huku akimtaka aingie uwanjani kubadili mwenendo wa mchezo na kusaidia timu kupata matokeo chanya.
Katika mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki wengi, Dodoma Jiji FC ilifanikiwa kuivunja rekodi ya Yanga ya kutofungwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Ushindi huo umeongeza presha kwenye mbio za ubingwa huku ukiifanya Dodoma Jiji kuendelea kuonyesha ushindani mkubwa dhidi ya timu kubwa za ligi.
Waziri amesema ana furaha kuwa sehemu ya ushindi huo muhimu, akieleza kuwa walifuata kikamilifu maelekezo ya benchi la ufundi jambo lililowasaidia kuutawala mchezo hasa eneo la kiungo.
“Kocha aliniambia nikacheze kama namba 10, nishuke chini kucheza mipira ili kuidhibiti nafasi ya katikati. Pia alinielekeza nikiona nafasi nikimbie nyuma ya mabeki wao, na hilo lilifanikiwa kwani nilifunga bao la ushindi,” amesema Waziri.
Akizungumzia kitendo chake cha kushangilia kwa nguvu baada ya kufunga dhidi ya timu aliyowahi kuichezea, Waziri alisema alichochewa na maneno ya shabiki mmoja wa Yanga aliyekuwa akimtukana alipokuwa akijiandaa kuingia uwanjani.
“Nilikerwa sana na yale matusi, ndiyo maana baada ya kufunga nikaenda kushangilia upande ule ule,” amesema mshambuliaji huyo.