Habari za michezo
PSG YATWAA UBINGWA WA TANO BACK TO BACK LIGUE 1
Vardo
May 14, 2026
1:55 pm
Paris Saint-Germain imefanikiwa kutwaa ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1 baada ya kuichapa Lens mabao 2-0.
PSG ilikuwa inahitaji pointi tatu tu ili kutwaa ubingwa huo ambao imekuwa kawaida kwao kufanya hivyo kwa miaka ya hivi karibuni.
Timu hiyo ambayo baadaye mwezi huu itacheza mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal ilifanikiwa kujipatia mabao yake kupitia kwa Khvicha Kvaratskhelia na Ibrahim Mbaye.
Ushindi huo umeifanya kuwa kileleni kwa tofauti ya pointi tisa ikiwa imebakiza mchezo mmoja ligi hiyo kumalizika.
Kwa sasa PSG imefanikiwa kutwaa makombe 14 ya Ligue 1, huku 12 wakiyapata miaka 14 iliyopita baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi na uongozi.
PSG ndiyo timu iliyotwaa makombe mengi makubwa msimu huu ikiwa pia imechukua UEFA Super Cup, FIFA Intercontinental na Ubingwa wa Ufaransa.
Timu hiyo inaweza kutwaa ubingwa mwingine kwa kuwa inakwenda kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal Mei 30 na kama itatwaa ubingwa itakuwa timu ya kwanza kwenye kipindi hiki kutetea kombe hilo.
Kwa upande wa Lens yenyewe ina uhakika wa kumaliza nafasi ya pili na kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2023/24.