Habari za michezo

INTER MILAN YATWAA UBINGWA WA COPA ITALIA

Vardo May 14, 2026 2:04 pm

Ikiwa zimepita siku chache baada ya kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Italia ‘Seria A’, Klabu ya Inter Milan imeendelea kufanya kweli safari hii ikitwaa Kombe la Copa Italia baada ya kuifunga Lazio mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa usiku wa jana Mei 13, 2026.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Olimpico jijini Roma, ilishuhudiwa mabingwa hao wapya wakipata mabao mawili katika kipindi cha kwanza yaliyoihakikishia timu hiyo nafasi ya kutwaa taji hilo.

Inter iliandika bao la kwanza dakika ya 14 baada ya kiungo wa Lazio, Adam Marusic kujifunga alipokuwa akitaka kuokoa mpira wa kona uliopigwa na kiungo wa Inter, Federico Dimarco.

Dakika ya 35 nahodha Lautaro Martinez aliandika bao la pili kwa Inter akimalizia kwa ustadi pasi aliyopewa na Denzel Dumfries.

Hata hivyo, Lazio walitengeneza nafasi kadhaa ili kurejea mchezoni lakini hazikuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Inter.

Vigogo hao wa Italia sasa wamefikisha jumla ya mataji 10 ya Copa Italia wakishika nafasi ya pili nyuma ya vinara Juventus wenye jumla ya mataji 15 ya mashindano hayo.Msimu huu umekuwa wa mafanikio kwa Inter ambao wanaongozwa na kocha Cristian Chivu wakifanikiwa kutwaa mataji mawili ya ndani ambapo wiki iliyopita walitangazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Seria A ‘Scudetto’ wakitwaa taji lao la 21.

PSG YATWAA UBINGWA WA TANO BACK TO BACK LIGUE 1 ALLARAKHIA APANDISHA TIMU ENGLAND, MNOGA AKIISAKA LEAGUE ONE