Habari za michezo

ALLARAKHIA APANDISHA TIMU ENGLAND, MNOGA AKIISAKA LEAGUE ONE

Vardo May 14, 2026 2:10 pm

SOKA la England linaendelea kushuhudia mchango wa wachezaji wenye asili ya Tanzania, huku Tarryn Allarakhia akiwa tayari ameandika historia kwa kuisaidia Rochdale A.F.C. kupanda kutoka National League (Daraja la Tano) kwenda EFL League Two (Daraja la Nne).

Wakati Allarakhia akisherehekea mafanikio hayo, Haji Mnoga akiwa na Salford City, wanakabiliwa na dakika 90 muhimu zitakazoamua kama wataendelea na safari ya kupanda EFL League One (Daraja la Tatu).

ROCHDALE

Rochdale imefanikiwa kupanda National League baada ya ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Boreham Wood F.C. katika fainali ya playoff iliyopigwa Mei 10, 2026.

Ushindi huo ulihitimisha msimu mzuri kwa klabu hiyo, ambayo ilitumia uzoefu wa wachezaji wake wa pembeni, akiwemo Allarakhia, kufanikisha ndoto ya kushiriki EFL League Two.

Ingawa hakuwepo kwenye mechi hiyo, lakini Allarakhia ana mchango wake ndani ya kikosi hicho.

Winga huyo wa kushoto mwenye uwezo wa kukimbia kwa kasi, kupiga krosi na kusaidia timu kubadilisha mchezo, huu ni msimu wa pili kuwa hapo alipotua 2024-2025 akitokea Wealdstone ambapo ndani ya misimu miwili alifunga mabao 11 kwenye mechi 56.

Akiwa na Rochdale msimu wake wa kwanza alifunga mabao manne kwenye mechi 43 na msimu huu amecheza mechi 30 akifunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao.

MUSTAKABALI WAKE

Pamoja na mafanikio hayo, hatma ya Allarakhia ndani ya Rochdale bado haijajulikana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mkataba wake unatamatika Juni 30, 2026. Hadi sasa, klabu hiyo haijatangaza rasmi mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.

Hali hiyo ina maana kuwa winga huyo anaweza kubaki, kuondoka kama mchezaji huru na kupata ofa kutoka klabu nyingine baada ya kuonyesha uwezo wake katika msimu huu wa mafanikio.

Kuna tetesi zinaeleza huenda Allarakhia akaondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na kocha wa timu hiyo, Jimmy McNulty.

WASIFU WAKE

Allarakhia ni mzaliwa wa Redbridge nchini London mwenye asili ya Tanzania, alianza safari yake ya soka katika akademi ya Leyton Orient. Akiwa kijana alipata nafasi ya kufanya majaribio katika kikosi cha Bournemouth na Norwich City, lakini hakufanikiwa kusajiliwa. Mwaka 2015 alijiunga na kikosi cha kwanza cha Aveley, kabla ya kuhamia Maldon & Tiptree mwaka 2016 ambako aliendelea kuonyesha uwezo wake kama winga hatari.

Ubora wake ulimfungulia mlango wa kusajiliwa na Colchester United mwaka 2017, ingawa alidumu kwa msimu mmoja kabla ya kuachwa.

Mwaka 2018 alisajiliwa na Crawley Town, ambapo pia alitolewa kwa mkopo Wealdstone na kufanya vizuri kwa kufunga mabao manne katika mechi 18. Baadaye alicheza Woking kwa msimu wa 2021-2022 kabla ya kurejea Wealdstone mwaka 2022.

Tangu kurejea kwake, Allarakhia alijijengea nafasi muhimu kikosini kwa mabao na mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji, hali iliyomfanya kuendelea kupiga hatua hadi kufikia mafanikio ya hivi karibuni ya kuisaidia Rochdale kupanda hadi EFL League Two.

MNOGA ANA KAZI KESHO

Wakati Allarakhia akifurahia kupanda daraja, Mbongo mwenzie Haji Mnoga anayekipiga Salford City, ana dakika 90 kesho za kuamua safari yao ya kwenda Wembley kupambania nafasi ya kupanda kama timu hiyo EFL League One.

Salford City inatarajiwa kucheza mechi ya marudiano ya playoff dhidi ya Grimsby Town, ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-1 ilioupata ugenini katika mchezo wa kwanza.

Matokeo hayo yameiweka Salford katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mbio za kupanda League One, lakini bado inahitaji kumalizia kazi nyumbani.

AMEKIWASHA

Mnoga amekuwa mmoja wa wachezaji wa kuaminika katika kikosi cha Salford City, msimu huu amecheza mechi 25 kwa dakika 1,697, akianza mara 20.

Mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza beki wa kulia, beki wa kati na winga wa kulia, ameonyesha ubora mkubwa kwenye eneo la ulinzi, jambo lililomfanya kuwa sehemu muhimu katika mfumo wa kocha.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Grimsby Town, Mnoga alicheza dakika zote 90 na kusaidia timu hiyo kupata ushindi muhimu.

WASIFU WAKE

Haji Mnoga alianza safari yake ya soka nchini England kupitia akademi ya Portsmouth F.C, aliyojiunga nayo mwaka 2008 akiwa bado kijana mdogo.

Alipitia ngazi zote za vijana za klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya kusaini mkataba wa kwanza wa kitaaluma mwaka 2018 na kupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa.

Baada ya kuitumikia kwa muda mrefu Portsmouth, Mnoga alitolewa kwa mkopo katika klabu mbalimbali za England zikiwemo Bognor Regis Town F.C, Bromley F.C, Weymouth F.C, Gillingham F.C. na Aldershot Town F.C, kabla ya kujiunga na Salford City F.C mwaka 2024 ambako anaendelea kucheza hadi sasa.

WAMEWAKILISHA

Katika kipindi ambacho Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inaendelea kutafuta ushindani wa kimataifa, mafanikio ya wachezaji kama Allarakhia na Mnoga yanaongeza matumaini ya kuwa taifa lenye hazina kubwa ya vipaji vinavyocheza nje ya nchi.

Kwa sasa, mmoja tayari amefanikisha ndoto ya kupanda daraja. Mnoga ambaye tayari ametanguliza mguu mmoja anasubiri hatma yake kesho jioni.

Kama mambo yataenda kama wanavyotarajia, Mei 15, 2026 inaweza kuwa siku nyingine ya historia kwa soka la Tanzania nchini England.

INTER MILAN YATWAA UBINGWA WA COPA ITALIA YANGA YAJIKUTA KWENYE WAKATI MGUMU, MOALIN AFICHUA TATIZO