Habari za michezo
SIMBA YAJIBU KIJEMBE CHA YANGA KUHUSU UWANJA
Vardo
May 14, 2026
2:24 pm
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema klabu hiyo haiwezi kuingia kwenye mashindano ya maendeleo kwa kulinganisha kile kinachofanywa na timu nyingine, akisisitiza kuwa kila klabu ina mipango na malengo yake tofauti.
Kauli ya Ahmed imekuja baada ya msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe kutoa kijembe kuelekea Simba kufuatia makubaliano ya Yanga kujengewa uwanja na mdhamini wao GSM Group.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Ahmed amesema maendeleo ya klabu hayawezi kufanywa kwa presha ya kushindana au kuiga kile kinachofanywa na wengine, bali yanapaswa kwenda kwa kufuata mipango maalum ya uongozi wa klabu husika.
Amesema Simba tayari ina miundombinu yake ikiwemo uwanja wa mazoezi, hivyo hawaoni sababu ya kuharakisha mchakato wa kujenga uwanja wa mechi kwa sababu tu kuna timu nyingine imeanza mradi huo kupitia mdhamini wake.
“Hatuwezi kushindana. Simba ina uwanja wa mazoezi, mbona wao hawana? Ukiangalia hata KMC FC na Singida Black Stars wamejenga viwanja vyao wakati timu nyingine zimeanza juzi tu,” amesema Ahmed.
Ahmed amesisitiza kuwa Simba itaendelea kufanya maendeleo yake kwa kufuata utaratibu na mikakati waliyojiwekea, huku akieleza kuwa lengo kubwa la klabu hiyo ni kuhakikisha kila hatua wanayochukua inaleta manufaa ya kudumu kwa timu badala ya kufanya mambo kwa mihemko ya ushindani.