KOCHA Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohammed ‘Mani Gamera’ ameamua kuachana na timu hiyo baada ya kumalizika kwa mechi ya hatua ya robo fainali ya Kombe la FA ambapo timu hiyo iliondoshwa na Mwenge kwa kufungwa bao 1-0.
Taarifa ilizozipata Mwanaspoti ni kwamba, uamuzi huo umekuja baada ya kudaiwa baadhi ya viongozi wa timu hiyo kumtolea maneno yasiyofaa na kumtuhumu kuwa hakuipa umuhimu mechi hiyo.
Wakati hayo yakiendelea, Mwanaspoti ilizungumza na Ofisa Habari wa Fufuni, Suleiman Ame ambaye alithibitisha kutokea kwa sintofahamu hizo, lakini hivi sasa uongozi upo kwenye mazungumzo ya kumrudisha kocha huyo kwani ameondoka bila ya baraka za timu.
Akielezea chanzo cha ugomvi huo, Suleiman alisema uongozi wa timu haukuridhishwa na kikosi kilichopangwa siku ya mechi hiyo kwani siyo kile kinachocheza mechi za Ligi Kuu Zanzibar.
Akijibu tuhuma hizo, Kocha Gamera alisema kama uongozi huo hawakuridhika na kikosi hicho walipaswa kusitisha awali kwa sababu lazima uongozi wa timu wapitie ili kubaini kasoro.
“Ninachohitaji aliyenikashifu ndiye aniombe msamaha kinyume na hapo sipo tayari kurudi kwa timu hiyo ambayo shukrani yake ni matusi baada ya yote niliyoitendea,” alisema.
Kocha huyo, alisema amechezesha kikosi namba mbili kwa sababu ya kuona mechi ngumu mbele yao zilizofuatana ikiwemo dhidi ya New King, KVZ na JKU ili kujihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kwani hivi sasa timu hiyo inashika nafasi ya tatu ikiachwa pointi mbili na kinara KVZ, zikibaki mechi sita.
Alisema, kinachomshangaza kuwa viongozi waliotoa kauli hizo za matusi hawafuatilii mwenendo wa timu, huku akibainisha kwamba, anatambua amefanya uamuzi mgumu kwa kipindi hiki lakini amelazimika kufanya hivyo kwani hajapendezwa na maneno yasiokuwa na nia ya kujenga. Kuhusu nani anasimamia timu kwa sasa, Ofisa Habari wa Fufuni, Suleiman Ame alisema: “Kwa sasa timu ipo chini ya Kocha Msaidizi, Suleiman Abdalla huku mipango na mazungumzo ya kumrudisha (Gamera) yakiendelea.”
NEW CITY YASISITIZA KUTOSHUKA DARAJA
NEW City baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Zafsa katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, imesema haiwezi kushuka kama wengi wanavyotarajia.
Hayo yamebainishwa na kiungo mkabaji wa timu hiyo, Hassan Rakwe Iddy wakati akizungumza na Mwanaspoti baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliochezwa Mei 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa B.
Kiungo huyo alisema: “Licha ya timu yetu kutokuwa katika nafasi nzuri ya ligi, bado hatutoshuka daraja msimu huu.” Rakwe alisema, awali malengo yao yalikuwa ni kurejea Ligi Kuu Zanzibar lakini imeshindikana kwa sababu walianza msimu vibaya kwa kupoteza mechi nyingi hali iliyowanyima fursa hiyo mapema na sasa wanapambana wasishuke.
Kiungo huyo alisisitiza kuwa, wanataka kuendeleza rekodi nzuri wakipania kutopoteza mechi tano zilizobaki dhidi ya Ujamaa, Kundemba, Black Sailors, Negro United na Sharp Boys, ili wajipange msimu ujao. “Tunawaomba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono katika michezo mitano iliyobaki ili tuweze kufanya vizuri kwani uwepo wao ni muhimu,” alisema.
New City ina pointi 30 ikiwa nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Unguja, huku Zafsa ikiendelea kusalia katika mstari mwekundu wa kushuka daraja ikikamata nafasi ya 14 na alama 24, zote zikibakisha michezo mitano.