Habari za michezo
ALGERIA YASAKA REKODI MPYA KOMBE LA DUNIA 2026
Vardo
May 15, 2026
9:26 am
CONSTANTINE, ALGERIA: TIMU ya taifa ya Algeria inajipanga kurejesha heshima yake katika soka la Afrika na dunia ikiweka malengo ya kufanya makubwa katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazotaraji kutimua vumbi kuanzia Juni 11 katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Miamba hiyo ya Kaskazini mwa Afrika maarufu ‘Mbweha wa Jangwani’ ni miongoni mwa mataifa ya kumi ya Afrika yatakayowakilisha bara hili katika fainali hizo za kubwa za dunia.
Algeria imefuzu mara tano kucheza Kombe la Dunia kwa nyakati tofauti ambazo ni 1982, 1986, 2010, 2014 na sasa 2026. imefanikiwa mara moja kufuzu kwa hatua ya mtoano, ilipofika katika hatua ya 16 bora mwaka 2014 nchini Brazili kabla ya kutolewa na Ujerumani waliokwenda kuwa mabingwa.
Algeria imekuwa ni timu ya Afrika yenye historia nzuri katika Kombe la Dunia tangu ilipoanza kushiriki baada ya fainali za mwaka 1982, Fifa walilazimika kubadilisha kanuni za mechi mbili za mwisho kuchezwa pamoja kwa sababu ya kitendo cha utata cha upangaji matokeo kilichofanywa na Ujerumani Magharibi dhidi ya Austria na kusababisha Algeria kushindwa kufuzu kwa raundi ya pili pamoja na kushinda mechi zake mbili za hatua ya makundi.
Kwa miaka mingi Algeria imekuwa kizalisha nyota wengi bora wanatikisa katika soka la Afrika na Dunia miongoni mwa wachezaji hao ni Rabah Madjer, Lakhdar Belloumi, Riyad Mahrez na Islam Slimani.
Algeria kwa sasa ipo nafasi ya 28 katika orodha ya viwango vya ubora vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vya mwezi Aprili 2026, jambo linaloonyesha namna taifa hilo lilivyorejea baada ya kupita katika nyakati ngumu.
HISTORIA YA ALGERIA
Historia ya soka la Algeria ina mizizi mirefu inayohusiana moja kwa moja na harakati za kupigania uhuru wa taifa hilo kutoka kwa wakoloni wa Ufaransa.
Kabla hata ya taifa kupata uhuru 1962, kulikuwa na timu maalum iliyoundwa na wapigania uhuru wa Algeria waliokuwa wakicheza soka ikiwa sehemu ya kuonesha utambulisho wa taifa lao.
Kuanzia 1957 hadi 1958 kulikuwa na kikosi cha ALN kilichoundwa nchini Tunisia. Hiki kilikuwa kikosi maalum kilichokuwa na dhamira ya kuitangaza Algeria kupitia mpira wa miguu wakati wa vita vya kupigania uhuru.
Baadaye kikosi hicho kilibadilishwa na timu maarufu ya FLN iliyojumuisha mastaa wengi waliokuwa wakicheza soka la kulipwa nchini Ufaransa. Wachezaji hao waliamua kuacha maisha yao ya kawaida ya soka na kujiunga na harakati za kisiasa kwa lengo la kuitangaza Algeria duniani kupitia mchezo wa mpira wa miguu.
Timu ya FLN ilicheza mechi nyingi za kirafiki katika mataifa mbalimbali ya Afrika na Asia. Ingawa FIFA haikuitambua rasmi timu hiyo kwa sababu Algeria ilikuwa bado chini ya ukoloni, mchango wake ulikuwa mkubwa sana katika kujenga utambulisho wa taifa na kuifanya dunia kutambua mapambano ya wananchi wa Algeria.
Baada ya kupata uhuru, Algeria ilianzisha rasmi timu yake ya taifa na mwaka mmoja baadaye ikajiunga na FIFA. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari mpya ya taifa hilo katika soka la kimataifa.
MWANZO WAO KIMATAIFA
Miaka ya mwanzo baada ya uhuru Algeria lilikuwa linajenga mfumo mpya wa michezo huku likijaribu kuendana na ushindani wa mataifa mengine ya Afrika yaliyokuwa tayari yameendelea kisoka.
Algeria ilicheza mechi yake ya kwanza rasmi 1963 na kuifunga Bulgaria mabao 2-1 mjini Algiers. Ushindi huo ulitoa matumaini makubwa kwa taifa hilo na kuweka nguvu mpya ya soka barani Afrika.
Katika miaka ya 1970 Algeria ilianza kuonyesha makali yake kwa kushiriki michuano mbalimbali ya Afrika na Mediterranean. Kipindi hicho ndipo majina ya nyota kama Lakhdar Belloumi na Rabah Madjer yalipoanza kutamba.
Taifa hilo lilifanikiwa kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Afrika 1978 na pia kushinda Michezo ya Mediterranean 1975, mafanikio yaliyoonyesha wazi kuwa Algeria ilikuwa imekuwa kisoka.
KOMBE LA DUNIA 1982
Kombe la Dunia la mwaka 1982 nchini Hispania ndilo lililobadili kabisa taswira ya Algeria katika ramani ya soka duniani. Hii ilikuwa mara ya kwanza taifa hilo kushiriki michuano hiyo mikubwa duniani.
Katika mechi yao ya kwanza, Algeria ilikutana na Ujerumani Magharibi iliyokuwa bingwa wa Ulaya wakati huo. Wengi waliamini Algeria ingepoteza kirahisi, lakini kilichotokea kilishtua dunia nzima.
Algeria iliifunga Ujerumani Magharibi mabao 2-1 katika moja ya matokeo makubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya Kombe la Dunia. Mabao ya Rabah Madjer na Lakhdar Belloumi yaliwafanya Mbweha Jangwani kuwa gumzo duniani kote.
Ushindi huo uliifanya Algeria kuwa taifa la kwanza la Afrika kuifunga timu ya Ulaya katika Kombe la Dunia, pia waliwafunga Mexico kwa mabao 3-2 na kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kushinda mechi mbili katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Hata hivyo safari yao ilimalizika kwa maumivu makubwa baada ya kile kilichoitwa ‘Aibu ya Gijon.’ Ujerumani Magharibi na Austria walicheza mechi iliyotuhumiwa kupanga matokeo ili kuhakikisha Algeria inaondolewa licha ya kufanya vizuri.
Baada ya sakata hilo FIFA ililazimika kubadilisha sheria na kuanza kupanga mechi za mwisho za makundi kuchezwa muda mmoja ili kuzuia upangaji wa matokeo. Hivyo Algeria ilibaki kwenye historia kama taifa lililosaidia kubadili mfumo wa Kombe la Dunia.
ENZI ZA MADJER NA BELLOUMI
Katika miaka ya 1980 Algeria ilikuwa na kizazi cha dhahabu kilichoongozwa na Rabah Madjer na Lakhdar Belloumi. Wachezaji hao Madjer alikuwa maarufu kwa uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao huku Belloumi akitambulika kama mmoja wa viungo bora kabisa kuwahi kutokea Afrika.
Kizazi hicho kiliiwezesha Algeria kushiriki Kombe la Dunia 1986 nchini Mexico ingawa hawakufanya vizuri, pia iliendelea kufanya vizuri katika mashindano ya AFCON.
UBINGWA WA AFCON 1990
Mwaka 1990 Algeria iliandika historia kubwa kwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza katika historia yake. Michuano hiyo ilifanyika nchini Algeria huku mashabiki wa taifa hilo wakijitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao katika kila mchezo.
Katika hatua ya makundi, Algeria ilionyesha ubora mkubwa baada ya kuichapa Nigeria mabao 5-1 katika moja ya ushindi mkubwa uliotikisa michuano hiyo. Ushindi huo uliwafanya wengi kuanza kuiangalia Algeria kama timu yenye uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa huo.
Mbweha Jangwani waliendelea kucheza kwa kiwango cha juu katika hatua zilizofuata hadi kufika fainali ambapo walikutana tena na Nigeria mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika ndani ya Uwanja wa 5 July 1962 mjini Algiers. Katika mchezo huo wa fainali, Algeria iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Chérif Oudjani katika dakika ya 38 na hivyo kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Afrika.
KIPINDI CHA ANGUKO
Baada ya mafanikio hayo, Algeria iliingia katika kipindi kigumu sana. Migogoro ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoathiri maendeleo ya michezo nchini humo.
Kwa muda mrefu Algeria ilishindwa kufanya vizuri AFCON na pia ilikosa nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa miaka mingi.
Kulikuwa na mabadiliko mengi ya makocha na kukosekana kwa mwendelezo wa mafanikio. Wakati mwingine taifa hilo lilionekana kupoteza kabisa mwelekeo wa kisoka.
KOMBE LA DUNIA 2010
Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, Algeria ilirejea tena Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Safari yao ya kufuzu ilikuwa ya kipekee sana hasa dhidi ya Misri. Mataifa hayo mawili yalikuwa kwenye ushindani mkali.
Baada ya timu hizo kufungana pointi, zikalazimika kucheza mechi ya mtoano nchini Sudan. Algeria ilishinda bao 1-0 kupitia Anthar Yahia na kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24.
Mashabiki wa Algeria walifanya sherehe kutokana na ushindi huo wa kihistoria.
Hata hivyo katika Kombe la Dunia la 2010 walishindwa kufunga bao lolote na kuondolewa hatua ya makundi.
HISTORIA MPYA 2014
Mwaka 2014 nchini Brazil, Algeria iliandika historia nyingine kubwa zaidi.
Ikiwa chini ya kocha Vahid Halilhodzic, Algeria ilionyesha kiwango bora. Walifungwa 2-1 na Ubelgiji katika mechi ya kwanza lakini baadaye wakaifunga Korea Kusini mabao 4-2.
Ushindi huo uliifanya Algeria kuwa taifa la kwanza la Afrika kufunga mabao manne katika mechi moja ya Kombe la Dunia.
Baadaye walitoka sare dhidi ya Urusi na kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Katika hatua hiyo walikutana na Ujerumani na kutoa upinzani mkubwa sana kabla ya kupoteza mabao 2-1 muda wa nyongeza.
Licha ya kutolewa, dunia ilikubali kuwa Algeria ilikuwa moja ya timu bora zaidi kutoka Afrika katika michuano hiyo.
ENZI YA RIYAD MAHREZ
Baada ya kizazi cha Belloumi na Madjer, Algeria ilipata nyota mwingine mkubwa duniani ambaye ni Riyad Mahrez.
Mahrez alijizolea umaarufu mkubwa akiwa Leicester City ambapo aliisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mwaka 2016 katika moja ya hadithi kubwa zaidi za soka duniani.
Kupitia uwezo wake mkubwa wa kucheza pembeni, kupiga chenga na kufunga mabao muhimu, Mahrez amekuwa sura ya Algeria kwa zaidi ya miaka 10.
Nahodha huyo mechi zaidi ya 113 akiwa na mabao 38 kwa timu ya taifa. Mahrez alikuwa mhusika mkubwa katika safari ya ubingwa wa AFCON 2019 ambapo bao lake la faulo dhidi ya Nigeria katika nusu fainali bado linakumbukwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
KOMBE LA DUNIA 2026
Algeria imefuzu Kombe la Dunia 2026 baada ya kufanya vizuri katika mechi za kufuzu Afrika.
Timu hiyo ilimaliza ikiwa kinara wa kundi lake huku ikionyesha ubora mkubwa wa kushambulia. Katika mechi 10 za kufuzu walishinda nane, sare moja na kupoteza mchezo mmoja pekee.
Walifunga mabao 24 na kuruhusu mabao manane, takwimu zinazoonyesha uimara wao.
Katika ratiba ya Kombe la Dunia 2026, Algeria ipo kundi J pamoja na Argentina, Jordan na Austria.
Mchezo dhidi ya Argentina unatajwa kuwa moja ya mechi zinazosubiriwa kwa hamu kubwa zaidi kutokana na historia ya Argentina katika soka la dunia.
NINI CHA KUFANYA 2026?
Changamoto kubwa kwa Algeria itakuwa namna ya kupambana na mataifa makubwa duniani huku ikijaribu kuvuka hatua ya makundi.
Kikosi chao kina mchanganyiko wa wachezaji uzoefu na vijana wenye vipaji vikubwa. Ikiwa Mahrez ataendelea kuwa kwenye kiwango kizuri na vijana kama Amoura, Gouiri na Maza wakaendelea kukua, Algeria inaweza kuwa moja ya timu zitakazoshangaza wengi.
Historia inaonyesha kuwa Algeria huwa hatari sana inapopewa nafasi ndogo. Ndivyo ilivyokuwa 1982 dhidi ya Ujerumani na 2014 walipoisumbua Ujerumani iliyokuja kuwa bingwa wa dunia.
Safari ya 2026 inaweza kuwa nafasi nyingine kwa Mbweha wa Jangwani kuandika historia mpya na kuonyesha tena nguvu ya soka la Afrika mbele ya dunia.