Habari za michezo
ANGEL NYIGU ALIVYOWAHESHIMISHA ZUCHU NA DIAMOND
Vardo
May 15, 2026
9:20 am
KATI ya dansa wa kike wanaofanya vizuri kwa sasa hapa nchini, ni pamoja na Angel Nyigu ambaye ametumika kuzipamba video nyingi za muziki na baadhi ya hizo zimekuwa na matokeo makubwa.
Angel amefanya kazi na wanamuziki wengi wa Bongofleva hadi sasa lakini kwa Zuchu na Diamond Platnumz, ndipo hasa amefanikiwa kuweka rekodi za kipekee zaidi!.
Kwa mujibu wa Angel, alianza rasmi kazi hiyo mwaka 2016, na hadi sasa ameshacheza katika video za muziki zaidi ya 30, kitu ambacho ni rekodi nyingine anayojivunia katika kazi yake hiyo.
Aliwahi kuwa dansa wa staa wa WCB Wasafi, Zuchu kwa miaka mingi ambapo mbali na kutokea katika video za nyimbo zake, pia walikuwa wakisafiri pamoja kwenda kwenye show mbalimbali za ndani na nje.
Ni Angel ambaye alicheza vizuri katika video ya wimbo wa Zuchu, Sukari (2021) akiwa kama dansa kiongozi katika mradi huo ambao uliweka rekodi Afrika kwa mwaka huo.
Hadi kufikia Desemba 2021, ndio ilikuwa video ya muziki iliyofanya vizuri zaidi YouTube Afrika ikitazamwa (views) mara milioni 60, huku ikifuatiwa na ile ya Wizkid na Tems, Essence (2021) iliyotazamwa mara milioni 53.
Machi 2024, video ya wimbo wa Zuchu, Sukari (2021) ikawa ya kwanza kutoka kwa msanii solo Tanzania na Afrika Mashariki kwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 100, pia hadi sasa ndio video pekee ya msanii wa kike iliyofanya hivyo.
Hata hivyo, nyuma ya mafanikio hayo kuna watu wengi na mmoja wapo ni Angel ambaye alionyesha ubunifu na uwezo mkubwa wa kucheza katika video hiyo iliyoongozwa na Director Kenny chini ya Zoom Extra.
Video nyingine ya Zuchu ambayo ipo mbioni kufikia rekodi ya kutazamwa YouTube mara milioni 100, ni ya wimbo wake, Kwikwi (2022), ambayo imefikisha milioni 91. Huku napo Anjel yupo na kucheza vizuri tu, hivyo naye atakuwa sehemu ya rekodi hiyo.
Mbali na Zuchu, Angel Nyigu amecheza (dance ) katika video za nyimbo za Diamond nyingi tu, baadhi ya hizo ni Sound (2019), Jeje (2022), IYO (2021) n.k.
Hapa napo Angel anastahili maua yake, kwani mnamo Agosti 2024, video ya Jeje nayo ilifikia rekodi ya kutazamwa YouTube mara milioni 100 ikiwa ni wimbo wa kwanza aliyoimba Diamond peke yake (solo) kufanya hivyo, huku akiwa ni msanii wa pili Afrika Mashariki baada ya Zuchu.
Ikumbukwe mwaka 2020, video ya Jeje nayo iliongoza kwa kufanya zaidi YouTube Afrika ikimaliza mwaka ikiwa imetazamwa mara milioni 40. Rekodi hii ni sawa na ile ya video ya Zuchu, Sukari (2021) ingawa hii namba zake zilikuwa juu zaidi.
Sasa Anjel amecheza katika hizo zote mbili ambazo ziliitikisa Afrika, na hadi sasa hakuna nyimbo nyingine kutoka kwa Zuchu, Diamond, wala wasanii mwingine wa Bongofleva aliyeweza kufanya kitu kama hicho.
Ni wazi kuwa Angel Nyigu kupitia kipaji chake cha dansa ambacho sasa ndio ajira yake rasmi, tayari ameacha alama kupitia kazi hizo na nyingine nyingi ambazo ameshirikiana na wasanii wengine.
Mbali na Zuchu na Diamond, Anjel amefanya kazi na mastaa wengine wa Bongofleva kama Vanessa Mdee, Harmonize, Rayvanny, Mimi Mars, Rosa Ree na Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music.
Hata hivyo, Vanessa Mdee ndiye mwanamuziki wa kwanza kumpa nafasi Anjel baada ya kuandaa shindano la kutafuta dansa wa kufanya naye kazi, ndipo akampa katika mchakato huo.
“Nilikutana na Angel mwaka 2016/17 alipokuja kufanya audition. Nilikuwa natafuta dancers wapya, na kipindi hicho madancer wakali wote Tanzania walikuja kushiriki,” anaeleza Vanessa na kuendelea.
“Nilikuwa pamoja na Msami na Head Dancer wangu, Diddy J, kama majaji. Ilikuwa ni vibe nzuri sana, na nilifurahia kushuhudia na kuwa sehemu ya tukio hilo. Miongoni mwa waliochaguliwa alikuwepo Angel Nyigu, na baada ya hapo tuliendelea kufanya kazi pamoja.”
“Mbali na kuwa na kipaji kikubwa na ubunifu wa hali ya juu, Angel alikuwa pia na msimamo wa kipekee. Aliweza kuona kabisa kwamba anapaswa kufanya kile alichokiamini na kweli alikifanya.”
“Leo hii naendelea kumuona akiipeleka dance mbali zaidi katika mataifa mbalimbali huku akiendelea kuboresha maisha yake. Ni jambo zuri sana kuona hilo. Najivunia wewe mtoto wangu, Mungu akubariki,” aliandika Vanessa katika Instagram.
Ikumbukwe Angel alishinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) kama Mchezaji Bora wa Kike 2023, huku akiwa tayari na tuzo mbili za kimataifa kutoka Kenya na Afrika Kusini.
Huyu ni mwanzilishi wa jumuiya ya Tanzania Dance ambayo imejikita katika kufundisha dansi watu wazima pamoja na watoto, na tayari wamewafikia watu zaidi ya 500 ambao huja na kuondoka.
Na idadi kubwa ya dansa kutoka Tanzania Dance walishiriki katika ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam mnamo Oktoba 2023.