Habari za Simba leo
Simba SC

WAKATI GSM AKIJENGA UWANJA YANGA….MO DEWJI AZIDI KUTAMBA DUNIANI….

admin May 15, 2026 5:44 pm

RAIS wa heshima wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji, ametajwa katika orodha ya TIME100 Philanthropy 2026 inayotolewa na jarida maarufu duniani la TIME, ikiwa ni kutambua mchango wake kwa jamii kupitia taasisi ya Mo Dewji Foundation.

Kutajwa kwa Dewji ambaye ameiongoza Simba kwa zaidi ya miaka minane katika orodha hiyo kunakuja wakati ambapo ameendelea kujijengea sifa kama mmoja wa wafanyabiashara vijana wenye mafanikio makubwa barani Afrika, huku akitumia sehemu ya utajiri wake kusaidia jamii kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kupitia Mo Dewji Foundation iliyoanzishwa mwaka 2014, Dewji amewekeza katika sekta za elimu, afya na maji safi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wenye uhitaji, hasa katika maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi na huduma muhimu za kijamii.

Jarida la TIME limemwelezea Dewji kama mmoja wa mabilionea vijana wa Afrika mwenye dhamira ya kutokomeza umaskini nchini Tanzania, akitumia fedha zake kusaidia miradi ya kijamii kwa zaidi ya miaka 20.

Katika safari yake ya biashara, Dewji aliyechangia mafanikio makubwa Simba akiiwezesha kutamba katika soka la kimataifa ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, alijiunga na kampuni ya familia ya MeTL Group iliyoanzishwa miaka ya 1970 na baba yake, ambapo alijikita katika kuzalisha bidhaa nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini Afrika Mashariki. Kampuni hiyo inajihusisha na sekta mbalimbali ikiwemo viwanda vya bidhaa za matumizi ya nyumbani, usafirishaji na mafuta.

Mbali na biashara, Dewji aliwahi kuwa mbunge kwa kipindi cha miaka 10, ambapo alitumia fedha zake binafsi kusaidia ujenzi wa shule, visima vya maji, vifaa vya kilimo pamoja na huduma za afya katika hospitali mbalimbali.

Kupitia Mo Dewji Foundation, zaidi ya maisha 635,000 yameguswa tangu mwaka 2001 kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi hiyo.

Katika sekta ya elimu, taasisi hiyo imeendelea kuwawezesha vijana wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma kupitia programu ya Mo Scholars Program, ambayo imelenga kukuza kizazi kipya cha viongozi. Hadi sasa zaidi ya vijana 250 wamepata ufadhili wa masomo kupitia mpango huo.

Mwaka jana pekee, taasisi hiyo ilipokea zaidi ya maombi 2,600 ya vijana waliotaka kujiunga na programu hiyo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 65 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kwa upande wa afya, taasisi hiyo imetoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa 75,000 kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali wa afya ili kusogeza huduma karibu na jamii zisizojiweza.

Katika sekta ya maji, zaidi ya wananchi 25,300 wamefikiwa na huduma za maji safi kupitia ujenzi wa visima na matumizi ya teknolojia za kisasa za usimamizi wa maji vijijini.

Mwaka 2016, Dewji aliahidi kutoa zaidi ya nusu ya utajiri wake kwa shughuli za kijamii kupitia mpango wa The Giving Pledge. Katika barua yake ya ahadi, Dewji alisema wazazi wake walimfundisha umuhimu wa kusaidia wenye uhitaji na kwamba jukumu la kila mwanadamu ni kuhakikisha jamii inakuwa bora kwa vizazi vijavyo.

Chini ya uongozi na udhamini wa mfanyabiashara huyo, Simba imefuzu mara sita robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika katika misimu ya karibuni, huku ikitinga fainali za Shirikisho Afrika msimu uliopita ikicheza na RS Berkane, ambapo ilifungwa kwa jumla ya mabao 3-1.

MERIDIANBET YAZITILIA WEPESI KAYA MBALIMBALI ZA TANDALE NINI KIMEMKUTA NABY CAMARA SIMBA…..HUU HAPA UKWELI USIOSEMWA…